Na Masanja Mabula,Pemba
SERIKALI ya mkoa wa kaskazini Pemba, imeelezea kusikitishwa na uchakavu wa makaro katika nyumba za maendeleo Mtemani wilaya ya Wete na kuagiza taasisi husika kuyafukia ili kuepusha uwezekano wa kutokea maradhi ya mripuko.
Mkuu wa Mkoa huo, Dadi Faki Dadi, alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watendaji wa Wizara ya Majenzi, Baraza la mji Wete,Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Shirika la Umeme Pemba.
Alisema ni vyema taasisi hizo kushirikiana pamoja na kuyafukia makaro hayo ambayo yamekuwa yakitiririsha maji machafu yenye vinyesi vya binadamu.
"Hili ni tatizo na linatakiwa kuchukuliwa hatua za haraka ili kunusuru afya za wakaazi wa nyumba hizi kupata maradhi ya mripuko,”alisema.
Katika hatua nyingine Dadi aliagiza migomba iliyopo bloke namba nne na tano yang’olewe ili kudumisha hali ya usafi.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Ofisa Mdhamini Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Pemba, Hemed Salim, alisema tatizo la nyumba hizo linakwamishwa na ufinyu wa bajeti.
Alisema tayari wizara imeomba fedha kwa ajili ya matengenezo ya nyumba hizo na kwamba wanatarajia kupatiwa fedha hizo kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
"Tatizo lipo na linasababishwa na ufinyu wa bajeti, lakini tunatarajia kwamba hali hiyo itaondoka katika kipindi hichi cha fedha kwani tumeomba fedha kwa ajili ya matengenezo ya nyumba hizi,” alisema.