Msemaji wa Timu ya Soka ya African Coast ya Upenja Wilaya ya Kaskazini “ B” Juma Mshamba akiomba radhi kwa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif hayupo pichani kufuatia uamuzi wa timu hiyo kuruhusu uwanja wao kutumika kwa mkutano wa hadhara wa chama cha upinzani ulioporomosha matusi dhidi ya mbunge huyo.
Mzee wa Timu ya African Coast Ali Soud akipokea mchango wa Mbunge wa Kitope Balozi Seif kwa ajili ya kulipa deni ya kambi ya timu hiyo pamoja na ada ya timu, kadi za wachezaji pamoja na Mrajisi wa michezo.
Mzee wa Timu ya African Coast Ali Soud akipokea mchango wa Mbunge wa Kitope Balozi Seif kwa ajili ya kulipa deni ya kambi ya timu hiyo pamoja na ada ya timu, kadi za wachezaji pamoja na Mrajisi wa michezo.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi Kepteni ya Timu ya Soka ya African Coast ya Upenja Ali Hassan Mipira,seti ya Jezi pamoja na Fulana za mazoezi kwa ajili ya wachezaji wa timu hiyo iliyomo ndani ya Jimbo lake.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ
Uongozi na wachezaji wa Timu ya Soka ya African Coast ya Kijiji cha Upenja umemuomba radhi Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi kufuatia uamuzi wa Timu hiyo kuruhusu kufanyika kwa Mkutano wa Hadhara wa Chama cha Upinzani uliozaa kashfa na matusi dhidi ya mbunge huyo.
Wachezaji hao waliomba radhi hiyo Mbele ya Mbunge huyo hapo katika Ukumbi wa Tawi la CCM la Kijiji cha Upenja kilichomo ndani ya Jimbo la Kitope Wilaya ya Kaskazini “B “ mkutano uliohudhuriwa pia na Wazee na baadhi ya viongozi waasisi wa CCM wa Kijiji hicho.
Akiwasilisha salamu hizo za kuomba radhi Msemaji wa Timu hiyo ya Soka ya African Coast Juma Mshamba alisema wachezaji na Viongozi wa clabu hiyo walifikia uamuzi wa kukutana na Uongozi wa Wazee wa Tawi hilo kwa lengo la kuomba radhi baada ya tukio hilo la mvua za matusi dhidi ya Viongozi wao.
Juma Mshamba alisema pamoja na nia safi ya Viongozi na Wachezaji hao ya kuruhusu Mkutano huo, lakini pia zilitumika mbinu za hadhaa kwa Viongozi wa upinzani kuahidi kuwapatia fedha za kuendesha klabu yao pamoja na kuwatengenezea uwanja wao mambo ambayo hakuna hata moja hadi sasa lililotekelezwa na chama hicho cha upinzani.
Juma Mshamba lifahamisha kwamba Viongozi na wachezaji hao wamemuahidi na kumuhakikishia Mbunge wao kwamba kitendo hicho kilichofanyika cha kuruhusu mikutano unayozaa kashfa kwa Viongozi katu wamethibitisha kwamba hakitarejewa tena katika maisha yao.
“ Mheshimiwa tunakubali na kuthibitisha kwamba tumeteleza katika maamuzi yetu ya ghafla na tunomba tueleweke kuwa mtoto anaponyea kiganja chake mzazi hachukui maamuzi ya kukikata bali hukisafisha kiganja hicho “. Alifafanua Juma Mshamba kwa niaba ya Viongozi na wachezaji wenzake.
Akizungumza na Wazee, Viongozi na wachezaji hao wa African Coast Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema tayari ameshawasamehe tokea wakati wa mshindano ya Jimbo la Kitope ya Kombe la ZAWEDA ambapo timu hiyo iliidhinishwa kushiriki kwenye mashindano hayo.
Alisema uwamuzi huo umechukuliwa na kamati ya mashindano hayo ikielewa wazi kwamba ushawishi wa viongozi wa upinzani ndio sababu iliyopelekea wanamichezo hao kuteleza.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa wanamichezo hao kujiepusha na vitendo vyote vinavyoashiriadalili za uvunjifu wa amani katika maeneo yao.
Balozi Seif alieleza kwamba ipo mifano ya wazi katika nchi mbali mbali Duniani inayoonyesha kuchezewa kwa amani na hivi sasa Mataifa hayo yametumbukia katika fadhaa na balaa jambo ambalo hata Vijana wa mataifa hayo wanashindwa kuendeleza michezo na burudani zao.
Alifahamisha kwamba amani inapotoweza popote pale jamii huchukuwa muda mrefu kuirejesha katika hali yake ya kawaida huku ikiacha makovu na simanzi miongoni mwa watu waliotetereka.
Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope aliwapongeza Vijana hao wa Kijiji cha Upenja kwa msimamo wao waliouonyesha wa kuendelea kukiunga mkono chama Tawala cha Mapinduzi.
Balozi Seif aliwataka wanamichezo hao kuzidisha juhudi katika harakati zao za kimichezo ili kujijengea msingi mzuri wa kupata ajira ndani ya sekta hiyo ambayo kwa hivi sasa inaonekana kuchukuwa eneo kubwa la ajira Duniani.
“ Mnapaswa kuendeleza michezo mkizingatia suala la nidhamu kama nilivyosisitiza kwenye fainali ya mashindano yetu ya Jimbo kombe la ZAWEDA na Uongozi wa Jimbo utakuwa tayari kuchukuwa jitihada za kusaidia changamoto zenu “. Alisema Balozi Seif.
Katika kuunga mkono jitihada zao za kuimarisha michezo Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope aliwahakikishia wanamichezo hao kwamba zile changa moto zinazowakabili likiwemo marekebisho wa uwanja wao yatafanyiwa kazi na Uongozi wa Jimbo hilo.
Naye Mke wa Mbunge huyo wa Kitope Mama Asha Suleiman Iddi aliwatanabahisha wanamichezo hao kuwa mbali na udanyanyifu wa baadhi ya watu wanaowatumia wanamichezo katika kushiriki kufanya maovu mitaani.
Mama Asha alisema maovu hayo huibuliwa ndani ya makundi ya vijana na wanamichezo kwa kutumiwa mwamvuli wa dini ingawa dini hizo misingi yake mikubwa ni kuimarisha amani na mshikamano miongoni mwa waumini wake.
Katika mkutano huo wa kuomba radhi Balozi Seif aliichangia Timu hiyo ya Soka ya African Coast ya Upenja Seti ya Jezi, Fulana za Mazoezi, Mipira, fedha taslimu shilingi Laki 625,000/- kwa ajili ya kulipa ada za sajili, Deni la kambi wakati wakiwa katika mashindano ya ligi ya Wilaya, kadi za wachezaji pamoja na fedha za mrajisi wa michezo.