WAPENZI wa nyimbo za zamani za taarabu asilia nchini, leo wanatarajiwa kupata burudani safi na ya aina yake kutoka kundi la Spice Modern Taarab, ndani ya ukumbi wa Safari Carnival uliopo Kawe, (opposite) na Clouds fm katika gate la kuingilia Escape 1.
Kwa kiingilio cha sh 5000 tu, kuanzia saa mbili usiku mpaka majogoo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Fabak Fashions, Asia Idarous Khamsin, ambao ni miongoni mwa wadhamini wa onyesho hilo, amewasihi wadau kujitokeza kwa wingi kuuenzi usiku huo kwa kukumbushiana enzi.
Asia Idarous alisema onyesho hilo maarufu kwa jina la ‘Old is Gold na Spice Modern Taarab,’ tayari limeanza kujizolea umaarufu kwa wadau ambapo wanakutana kwa pamoja na kufurahia shoo hizo.
“Kwa kiingilio cha sh 5,000 tu, wadau watafurahia shoo kabambe kutoka kwa Spice Modern Taarab kwa kupata nyimbo za mwambao hasa zile zilizokuwa zikipendwa, kuanzia saa 2 usiku hadi saa 8 usiku,” alisema Asia Idarous.
Spice Modern taarab wanatamba na nyimbo mbalimbali ambapo watapiga na nyimbo zilizowahi kutamba miaka ya zamani kama ambazo zimekuwa gumzo kipindi hicho ni pamoja na ‘Pendo kitu cha hiari’, ‘Dunia ina fisadi,’ ‘Kasha’ na nyingine nyingi.
Aidha aliwataja Wadhamini wengine katika usiku huo wa taarabu asilia ni Times FM, Fabak Fashions na Safari Carnival.