STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 03 Agosti , 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Lindi kwa utekelezaji mzuri wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Ndg. Ludovick Mwananzila hivi karibuni Dk. Shein alisema ametiwa moyo na takwimu za utekelezaji wa programu zilizo chini ya Mpango huo kwa mkoa wa Lindi.
“Nina matarajio makubwa na mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa kutokana na namna taarifa ya Mkoa ilivyoeleza”alisema.
Dk. Shein alieleza kuwa ushirikiano kati ya viongozi wa mkoa na wananchi umeweza kuufanya mkoa huo kupata mafanikio makubwa yakiwemo katika kilimo cha mazao ya biashara na chakula ambapo kwa msimu uliopita mkoa huo uliweza kupata ziada ya chakula ya tani 192,964.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa Lindi, mkoa huo msimu wa mwaka 2013/2014 ulivuna jumla ya tani 393,965 za mazao mbalimbali ya chakula ikiwa ni ziada ya tani 192,964.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapa pole wananchi wa Mkoa wa Lindi kwa mafuriko yaliyosababishwa na kujaa kwa mto Lukuledi na kupelekea kukatika kwa madaraja ya Mtama na Nyangao hivyo kuathiri shughuli zao za kila siku.
Hata hivyo alieleza kusikitishwa kwake na taarifa za kuwepo kwa matukio sita ya mauaji ya wanawake huko katika wilaya ya Nachingwea na kueleza kuwa vitendo kama hivyo vinalifedhahesha taifa.
Katika taarifa yake kwa Rais wa Zanzibar, Mkuu wa Mkoa Lindi Ludovick Mwananzila alieleza kuwa mbali ya kupata ziada ya chakula kwa msimu uliopita, Mkoa wake kwa miaka miwili mfululizo umeweza kupita lengo la makusanyo ya fedha za ndani.
Alifafanua kuwa kwa mwaka 2012/2013 mkoa uliweza kukusanya shilingi bilioni 7,196,096,480/= ikiwa ni asilimia 101.95 ya lengo la shilingi bilioni 7,058,458,000/= wakati kwa mwaka 2013/2014 ulikusanya 7,332,850,085/= sawa na asilimia 102.9 kutoka lengo la 7,233,604,000/=.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huyo,ukusanyaji huo mzuri wa mapato umesaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya elimu, afya, uvuvi, usafirishaji ikiwemo ujenzi wa kituo cha mabasi pamoja na mabanda ya maonesho ya nanenane.
Kuhusu kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato alieleza kuwa pamoja na mambo mengine kunatokana na ukusanyaji mzuri wa mapato na mwitikio mkubwa wa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi ghalani.
Sababu nyingine ni kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya biashara ikiwemo ufuta na bei nzuri ya zao hilo, kuimarika kwa mazingira ya utendaji kazi kwa kujenga ofisi za Kata na kuongezeka shughuli za utafiti na uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo gesi, madini na utalii ambapo wahusika wanalipa mirahaba na ada mbalimbali.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alikuwa mkoani Lindi kwa ziara ya siku moja ambako alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Maonesho ya Wakulima ikiwa ni sehemu ya Uzinduzi rasmi wa Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane mwaka huu ambayo yanafanyika kitaifa mkoani Lindi.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822