Na Bashir Nkoromo
JESHI la Polisi nchini limechukua hatua za kujiimarisha zaidi katika kuukabili uhalifu kisasa zaidi kwa kuamua kuviunganisha vituo vyake vikubwa kwenye mtandao wa mawasiliano katika mkongo wa taifa.Kufuatia hatua hiyo, ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano hayo umeshaanza kwenye vituo vikubwa vya polisi katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Zanzibar na jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kotes (T) Limited iliyopewa na jeshi la polisi kutengeneza mindombinu hiyo, Max Komba, alisema, ujenzi huo ulianza kituo cha polisi Kurasini, Chuo cha Polisi Chang'ombe na Oysterbay ambako ujenzi wake ulitarajiwa kukamilika jana.
Komba alisema, kampuni yake imepewa kufanya kazi katika mikoa hiyo kwa wiki tatu, tangu ilipoanza Julai 27 mwaka huu kwa mujibu wa mkataba, na ujenzi unatakiwa uwe umekamilika ifikapo Agosti 20 mwaka huu.
Akizungumzia mradi huo, msemaji wa polisi, Advera Senso alisema, mradi huo ukikamilika utasaidia kupunguza gharama na muda mwingi ambao jeshi limekuwa likitumia kufuatilia kumbukumbu za kuwatambua wahalifu.
Alisema, kupitia mtandao huo, vituo vilivyounganishwa vinaweza kupata taarifa na kuziona kwa wakati mmoja na kwa haraka zaidi, jambo ambalo litawezesha kumbaini mhalifu haraka zaidi na kuwa na ushahidi wa kutosha baada ya kumnasa.