Na Farida Msengwa, Morogoro
WASHTAKIWA watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji ya mtoto Nasra Rashid Mvungi, wamebadilishiwa Hakimu baada ya hakimu wa mwanzo kupata dharura.
Washtakiwa hao ambao kesi yao imekuwa ikifikishwa na kutajwa mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi wa mahakama ya hakimu Morogoro, Mary Moyo, walipandishwa kizimbani mbele ya hakimu Agripina
Kimanze na kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Kufuatia hali hiyo, washtakiwa hao walichelewa kupanda kizimbani tofauti na nyakati nyingine, hali iliyoonekana huenda ilisababishwa na mabadiliko hayo.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi,Aminatha Mazengo, aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kwamba jalada bado lipo kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali, hivyo kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Mahakama imeridhia ombi hilo na kupanga Agosti 20 mwaka huu kufikishwa tena kwa kesi hiyo kwa ajili ya kutajwa, kutokana na mahakama hiyo kukosa uwezo kisheria kusikiliza shitaka la mauaji.
Kesi hiyo ya mauaji inawakabili washtakiwa watatu akiwemo baba mzazi wa mtoto Nasra,Rashid Mvungi pamoja na waliokuwa walezi wake, Mariam Said na mumewe Mtonga Omary, ambao awali walikuwa wakikabiliwa na shtaka la kula njama na kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya marehemu kabla ya shitaka lao kubadilishwa baada ya mtoto huyo kufariki.