Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Magaidi wawalenga wanawake

$
0
0
Na Joseph Ngilisho,Arusha
UGAIDI wa aina yake umegubika jiji Arusha, ambapo watu wasiofahamika wanaotumia usafiri wa pikipiki, wanawashambulia kwa risasi wanawake hasa wenye usafiri wa magari bila kupora chochote.

Tayari wanawake watatu wamepigwa risasi katika maeneo tofauti jijini hapa huku mmoja kati yao aliyetajwa kwa jina la Shamim Rashird Yulu (30) mkazi wa Mbauda akipoteza maisha.

Marehemu alipigwa risasi ya shingo na anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwao Mbauda.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, alisema mashambulizi hayo ni ya kigaidi kwani wahusika baada ya kushambulia hawachukui chochote na wamekuwa wakiwalenga wanawake wenye magari pekee.

Akizungumzia shambulizi lililosababisha kifo, alisema limetokea juzi majira ya saa 3:00 usiku katika eneo la Sakina kwa Iddi wakati marehemu akijaribu kuingia nyumbani kwake.


Alisema marehemu alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Saloon yenye namba za usajili T506 BYA na kwamba alipofika eneo hilo watu wasiofahamika wakiwa na pikipiki walimpiga risasi shingoni na alifariki muda mfupi katika hospitali ya Selian.

Aidha katika tukio jingine mwanamke mwingine ambaye ni mke wa Mkurugenzi wa Shirika linalotetea haki za wafugaji la Pingos, Flora Porokwa, amelazwa hospitali ya Seliani baada ya kupigwa risasi kwapani iliyotokezea mgongoni na kuacha jeraha kubwa.

Mwanamke huyo alisema baada ya kufika eneo la kwa Iddi akiwa na gari lake aliona watu wawili wakiwa na pikipiki wakimzuia kwa mbele wakati akijaribu kukata kona ya kuingia bara bara ya vumbi ili aelekee nyumbani kwake.

Alisema mmoja wao  alimfuata na kumpiga risasi bila kuchukua chochote.

Tukio kama hilo limetokea eneo la Olasiti ambapo mwanamke mmoja asiefahamika jina alijeruhiwa kwa risasi na amelazwa hospitali ya mkoa ya Mount Meru akiendelea na matibabu.

Kamanda Sabas alisema tayari jeshi la polisi limeanza mazungumzo na wadau mbali mbali wakiwemo wafanyabishara kuangalia uwezekano wa kufunga kamera za CCTV kwenye mitaa mbali mbali jijjini hapa, zitakazosaidia kupunguza matukio ya kihalifu.

Wakati huo huo watu watatu wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za ugaidi huku mmoja aliyetajwa kwa jina la Adamu Musa Pakasi (34) mkazi wa Siwandeti wilayani Arumeru,akikutwa na bunduki ya kienyeji inayotumia risasi za short gun.

Alisema mbali na silaha hiyo pia alikutwa na risasi 38 za short gun,mafuta ya kusafishia bunduki na ganda moja la risasi.

Alisema watuhumiwa hao wanahusishwa na mtandao wa kigaidi wa kuripua mabomu na kwamba silaha hizo ni sehemu ya silaha zilizokuwa zikitumika kwenye uhalifu na uripuaji wa mabomu.


Mtuhumiwa huyo alikutwa na silaha hiyo pamoja na risasi zikiwa kwenye mfuko wa nailon nyumbani kwake na kwamba polisi itawafikisha mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>