STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 14 Agosti, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amempelekea salamu za pongezi Rais wa India Mheshimiwa Shri Pranab Mukherjee kwa kutimiza miaka 68 ya uhuru wa nchi hiyo.
“Inanipa furaha kutumia fursa hii adhimu kukutumia wewe binafsi Mheshimiwa Rais na kupitia kwako kwa wananchi wa India salamu za pongezi kutoka kwangu na kutoka kwa wananchi wa Zanzibar kwa kusherehekea miaka 68 ya Uhuru wa nchi yenu ” salamu hizo zimeeleza.
Katika salamu hizo Dk. Shein amebainisha kuwa wananchi wa Zanzibar wanajivunia uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yao na wananchi wa India na kwamba azma yao ni kuona uhusiano na ushirikiano huo unazidi kuimarika siku hadi siku.
Aliongeza kuwa wananchi wa Zanzibar wanafarijika kuona kuwa India imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika kipindi cha miaka 68 ya uhuru wake kutoka kwa wakoloni na kwamba maendeleo hayo yamekuwa yakiwanufaisha pia wananchi katika mataifa mengine.
“Kwa hiyo ninachukua fursa hii kuwasalimu ndugu zetu wa India katika siku hii muhimu na adhimu na kuwatakia maendeleo zaidi siku zijazo huku tukitarajia kuongeza kasi ya ushirikiano kati ya nchi zetu na watu wake” Dk. Shein alimalizia salamu zake.
.............................. .........
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pongezi Waziri Mkuu wa India Mheshimiwa Narendra Modi kwa kuadhimisha miaka 68 ya uhuru wa India.
Katika salamu zake hizo Dk. Shein amesema yeye binafsi na wananchi wa Zanzibar wanayo furaha kuungana na Mheshimiwa Narendra na ndugu zao wananchi wa India katika kusherehekea siku ya uhuru wa nchi hiyo.
“Tunatambua hatua kubwa ya maendeleo iliyofikia India tangu kupata uhuru wake na mbali ya maendeleo hayo kuwanufaisha wananchi wake tunashukuru kuona kuwa wakati wote India imekuwa tayari kuona maendeleo hayo yanawafikia pia watu wa mataifa mengine” amesema Dk. Shein.
Ameeleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanathamini sana uhusiano wa kihistoria uliopo kati yao na India pamoja na ushirikiano katika nyanja mbalimbali na kueleza matumaini yake kwa uhusiano huo kuzidi kuimarika katika siku zijazo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ametumia fursa hiyo kumtakia afya njema na maisha marefu Waziri Mkuu wa India Mheshimiwa Narenda Modi.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822