Na Salim Said Salim
KILA zama zina mambo yake, mazuri na mabaya. Zama tulionazo Zanzibar sasa ni za kusikitisha kwa vile ukienda sokoni, kwenye kituo cha daladala au katika baraza za kahawa kinachosikika ni kilio cha kuwasikitikia watoto.
Huyu analamikia ubakaji wa watoto, yule anaelezea ukuaji wa utoro katika shule nyingi na wengine wanasikitikia ajira wanazofanya watoto katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba ambazo zina athari mbaya kwa afya ya watoto na maisha ya hapo baadaye.
Kila mtu amekuwa hodari wa kutupa lawama upande mwengine, kama vile yeye hausiki na mtatizo haya yaliyoikumba jamii ya watu wa Zanzibar.
Hata Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, hivi karibuni wakati akihutubia baraza la Idd, ameelezea masikitoko yake juu ya namna ambavyo baadhi ya watu walivyojikita kuwafanyia unyama watoto wadogo na kutojali haki zao za msingi za kupata elimu na maisha.
Ukweli ni kwamba suala la haki za watoto kupuuzwa, mazingira ya maisha ya watoto wengi yakiwa yanatishiwa na na ubakaji na watoto wanaobakwa kutotendewa haki na vyombo vya dola na mahkama, kulazimika au kuingizwa katika ajira zinazowaathiri kiakili na kimwili na baadaye katika maisha yao ni kubwa kuliko linavyoangaliwa.
Orodha ya ajira zinazoonekana sana kwa watoto Visiwani ni ndefu. Miongoni mwao na ambazo zinazopelekea watoto wengi kutoroka shule na pia kuwaathiri kiakili na kimwili ni ndefu. Miongoni mwao ni: Uvunjaji mawe na kokoto kwa ajili ya ujenzi (zaidi kisiwani Pemba), kuchunga ng’ombe na mbuzi, kupara samaki, kupakia na kupakua mizigo bandarini na kwenye daladala, kuuza vyakula kama samaki, chapati na madazi (wengine huzunguka na vyakula hivi mitaaani).
Pia upo uvuvi na uchokoaji wa pweza, kusafirisha abiria na mizigo kwa ngalawa na mitumbwi kwenye vivuko.
Kwa ujumla zipo sheria nyingi Zanzibar za kuwalinda watoto na kuwawajibisha watu wanaowafanyia vitendo vya ubakaji au kutumia hadaa za kuwaajiri.
Lakini kuwa na sheria nzuri kwenye vitabu ni jambo moja na kuhakikisha sheria ziliopo zinafanya kazi kama ilivyokusudiwa ni jambo jingine.
Kwa kweli ukifanya uchunguzi utaona vipo vikwazo vingi vya wazi na vilivyojibanza katika familia, jamii, viongozi wa kisiasa na dini na katika vyombo vya sheria vinavyochangia kutomhakikishia mtoto wa Zanzibar maisha ya salama, raha na furaha.
Hali inakuwa mbaya zaidi kwa watoto mayatima na wale ambao wametelekezwa na wazazi, hasa baba zao. Mengine ukisimuliwa juu ya maisha ya shida dhiki na ya hatari yanayokabili baadhi ya watoto wa Visiwani huwezi kuamini ukizingatia sifa iliopata Zanzibar kwa miaka mingi ya kuwa watu wake ni waumini wazuri wa dini, wa pole, wacheshi kwa wakubwa na wadogo na makaimu.
Kwa ufupi ukisikia baadhi ya matokeo utasema wema wa watu wa Zanzibar umeshakwenda arijojo. Siku hizi imekuwa kawaida kusikia madai ya baadhi ya wakubwa kutumia vibaya madaraka yao na wenye fedha kutumia pochi zao kuzizima kesi za udhalilishaji wa watoto.
Kwa maana nyingine rushwa inatoa uthibitisho kuwa adui wa upatikanaji wa haki, ikiwa pamoja na ile ya watoto. Tafiti za Chama cha Waaandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar, taasisi mbali mbali za kiraia na vyombo vya habari zinaonyesha wimbi la ajira kwa watoto ni kubwa na vitendo vya kubaka watoto vimekuwa kwa kasi ya kusikitisha na kutisha katika karibu kila pembe ya Visiwani, mijini na vijijini.
Kwa bahati mbaya sehemu kubwa ya vitendo vya ubakaji hufanywa na watu wenye uhusiano wa karibu na watoto waliofanyiwa ukatili huu. Wahusika wengine ni walimu na viongozi wa dini ambao jamii huwatarajia kuwa mfano mzuri kwa jamii.
Uchunguzi wa kesi za ubakaji nao ni tatizo. Kesi nyingi huchukua muda mrefu na kumekuwepo na tuhuma za ubabaishaji na kuwakinga baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika na ubakaji.
Mara nyengine, kwa mujibu wa taarifa mbali mbali, pamekuwepo madai ya baadhi ya jamaa kuwasamehe waliowafanyia maovu watoto wao au kuwa tayari kupokea kitu kidogo ili sheria iisichukue mkondo wake.
Lakini lilio baya zaidi ni kuwa hata baadhi ya kesi ziliosikilizwa mahakamani na kuamuliwa kutolewa fidia basi upande wa walalamikaji hufanyiwa dhuluma ya aina nyingine.
Kila siku ahadi za kuwepo mchakato kupitia sheria ili kuzirekebisha…kwa vile adahabu zimepitwa na wakati. Kwa mfano katika kesi moja ya ubakaji kisiwani Pemba ilitolewa hukumu ya faini ya sh. milioni moja na laki saba.
Kati ya fedha hizo mahakama iliamua aliyetendewa ukatili huo apewe sh. laki nne tu kama fidia.
Hapa mtu unajiuliza busara gani ilitumika hata huyo aliyetendewa ukatili huo apewe sehemu ndogo tu ya fedha hizo?
Lakini linalosikitisha zaidi ni mpaka wiki iliopita wazazi wa huyo mtoto walikuwa hawajapewa fedha hizo.
Ninaamini ni busara kama fedha zote, ijapokuwa kidogo, zinazoamuliwa kuwa ndio faini, zikatolewa kwa familia ya mtoto aliyebakwa kwani ukweli ni kuwa hakuna kiwango cha fedha kinachoweza kufidia kitendo cha ubakaji ambacho humuathiri mtoto kimwili na kiakili.
Jingine linalozusha mjadala ni kwa nini jamaa aliyefanya unyama kwa huyo mtoto asipewe adhabu kali zaidi kwa vile alimharibia maisha huyo mtoto aliyembaka?
Tatizo jingine liliopo Zanzibar ni kwa jamii kuwa na muhali wa kutowafichua wabakaji na hata kuwalinda mitaani na mahakamani.
Huu sio utamaduni mzuri hata kidogo kwani mwenendo huu wa kuwaonea muhali wabakaji unawapa nguvu watu (kama wanastahili kuitwa hivyo) wanaowafanyia uchafu watoto kuendelea na tabia yao hii ya kinyama.
Watu wazuri hulindana kwa mema na sio kwa ushenzi kama huu wa kubaka watoto.
Viongozi wa dini nao waelewe kuwa wanao wajibu wa kuwakumbusha waumini wao haki za mtoto na sio tu kujikita katika ibada kwani dini zote zinasisitiza wajibu wa kila mtu kumlinda mtoto wake na wa mwenzake.
Vile vile ipo haja ya kuangalia upya tabia, mbali ya sifa za elimu kwa walimu wetu wa shule na madrasa kwani baadhi yao wamedaiwa kuwa mstari wa mbele kuwaharibu watoto wanaotarajiwa kuwasomesha.
Karibu kila siku tunasikia ahadi za viongozi kuwa mchakato wa kurekebisha sheria ili adhabu kali zitolewe kwa wabakaji upo mbioni.
Kwa hakika inasikitisha kuona miswaada ya sheria yenye utashi wa kisiasa hutayarishwa kwa kasi ya aina yake na hata kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi kwa hati ya dharura.
Lakini marekebisho ya sheria ili kuhakikisha watoto wanalindwa na washenzi wanaowafanyia unyama wa kuwabaka huwa ya mwendo wa konokono, tena kama aliyekuwa mwenye ulemavu unaompunguzia kasi ya kutembea.
Wakati umefika kwa watu wa Zanzibar kujitathmini upya na kuhakikisha wanakomesha vitendo vya kubaka watoto na kuwapa ajira zinazopelekea kukosa masomo na kuathiri afya zao na maisha ya baadaye.
Mwenendo wa huyu kuilaumu serikali, yule kuikandia polisi na mwengine kuzilaumu mahakama hausaidii kwani inakuwa sawa na kutwanga maji ndani ya kinu.
Ni lazima pawepo mkakati utaohakikisha watoto wanalindwa na kupatiwa haki zao na wale wote wanaowafanyia dhuluma au kuwadhalilisha wanawajibishwa kisheria.
Wahenga wanasema ukichelewa mwana kulia…utalia wewe, lakini kwa suala la ubakaji wakichelea wabakaji kuteseka jamii nzima itaumia.
Chanzo : Tanzania Daima