Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Shirika la Biashara la Taifa ZSTC limeandaa Programu ya Maonesho ya Sinema katika Vijiji vya Unguja kwa lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya uimarishaji wa Zao la Karafuu nchini.
Maonesho hayo ambayo yatakuwa yakifanyika muda wa usiku katika vijiji mbali mbali yatatoa fursa pia kwa Wananchi kuwauliza Maafisa wa ZSTC maswali yanayohusu kuimarisha zao hilo la biashara nchini.
Akizungumza katika maonesho hayo yaliyoanza huko katika kijiji cha Gamba Mkoa wa Kaskaini Unguja Meneja Mawasiliano wa ZSTC Ally Mohamed Ally amesema Progaramu hiyo itasaidia kuwajengea uelewa Wanachi na Ari ya kuendeleza Kilimo cha Zao la Karafuu katika Vijiji vyao.
Amesema Serikali ya Mapinduzi inachukua juhudi mbali mbali za kuliendeleza Zao la Karafuu lakini baadhi ya wananchi wamekuwa hawafahamu juhudi hizo hivyo ZSTC wameamuwa kuwafuata vijijini kwao ili kutoa elimu bora ya kilimo cha zao hilo.
“Serikali inafanya juhudi kubwa sana za kuimarisha Zao la Karafuu lakini baadhi ya Wakulima hawalifahamu hilo lakini kupitia maonesho haya tunaamini wananchi wengi wataelewa na kuisaidia Serikali katika kuwaelimisha wenzao ili kwenda sambamba na Sera ya Serikali ya kuliimarisha zao hilo” alisema Ally.
Kwa upande wao Wanakijiji wa Gamba wamelishukuru Shirika la ZSTC kwa kubuni njia hiyo ambayo inaamsha hamasa na ari ya kushiriki katika kuliimarisha Zao hilo.
Akizungumza mara baada ya Maonesho hayo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazalishaji Karafuu Jimbo la Chaani Haji Khamis Faki ameliomba Shirika hilo kufanya Maonesho hayo na Semina za mara kwa mara ili waweze kupata elimu zaidi.
Amesema kukosekana kwa Elimu na hamasa ya mara kwa mara ndiko kunakopelekea wananchi kupuuza upandaji wa Mikarafuu katika Vijiji hivyo.
Aidha amelishauri Shirika la ZSTC kuzidisha mashirikiano na Wanavijiji hasa katika ugawaji wa miche ya Mikarafuu ili iwafikie walengwa wanaostahiki kupata Miche hiyo.
“Ukweli unabaki kuwa hata hiyo miche ya Mikarafuu haitufikii sijui wanapelekewa nani kwa hiyo tunaiomba Serikali kupitia Shirika wanapogawa Miche basi watafute njia nzuri ya kumpatia kila mkulima anayestahiki kupata” Alisema Haji.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Wizara Badru Kombo Mwemvura amesema ushauri uliotolewa na Wanakijiji hao wataufanyia kazi na kwamba Miche ya Mikarafuu itasambazwa na kuwafikia wanakijiji hao kadiri itakavyowezekana.
Katika Maonesho hayo Wananchi wa kijiji cha Gamba waliweza kujifunza kupitia maigizo Umuhimu wa Zao la Karafuu nchini, Namna mzuri ya kuzianika na kuzitayarisha Karafuu kwa ajili ya kuziuza.