Na Laylat Khalfan
POLISI jamii Mkoa wa Mjini Magharibi, imesema kuoengezeka kwa makosa ya uhalifu Mkoani humo kunachangiwa na Wananchi kuwaficha wahalifu wa makosa hayo.
Kamanda Mkaguzi wa polisi jamii mkoa wa Mjini Magharibi, Mohammed Ramadhan, alisema hayo katika ziara ya kutembelea vituo vya ulinzi shirikishi katika shehia za mkoa huo.
Alisema kuwa baadhi ya Wananchi wana tabia ya kufumbia macho matatizo yanayojitokeza kwenye maeneo yao yakiwemo utumiaji wa dawa za kulevya na vitendo vya ubakaji.
Aidha alisema kuwa endapo Wananchi watakuwa na ushirikiano wakutosha na jeshi la polisi basi kwa kiasi kikubwa uhalifu utapungua katika jamii na kuweza kuleta maendeleo.
Kamanda huyo alisema Wanachi wanapaswa kushirikiana na jeshi la polisi katika kukomesha vitendo viovu kwa kutoa taarifa za watu wanaowatilia mashaka.
Aidha alifahamisha makosa mengine yaliyojitokeza ni pamoja uuzaji wa dawa za kulevya mtaa wa Kundemba ambao unachukuliwa kama soko kuu la biashara hiyo.
“Ni jambo la kushangaza sana jinsi ulivyo mtaa wa kundemba yaani kazi yao kubwa ni kujishirikisha na mambo maovu ambayo yanasababisha kurudisha nyuma mendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla”alisema Mkuu huyo.
Alieleza polisi jamii amejipanga kuweka mikakati madhubuti ambayo itasaidia kukomesha vitendo vya uvunjani amani nchini.