Na Mwandishi wetu
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umewataka viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), waache kuzungumzia kesi zilizoko mahakamani.
Umesema kuwa kuzungumzia kesi inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mansoor Yussuf Himid ni kuingilia uhuru wa mahakama na kinyume cha utawala bora.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamadu Shaka, alipozungumza na waandishi katika ukumbi wa Gymkhana mjini Unguja.
Shaka alisema haikuwa muafaka kwa Katibu Mkuu wa CUF, Maaalim Seif Sharif Hamad na mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Ismail Jussa Ladhu, kutumia jukwaa la kisiasa kuzungumzia kesi hiyo.
Alisema shtaka linapokuwa mahakamani hairuhusuwi kulizungumzia kwani kufanya hivyo kunaweza kuishinikiza au kuizuia mahakama isifanye kazi kikamilifu.
Katika hatua nyingine Shaka, alisema CCM haina mpango wa siri wa kugawanya majimbo ya uchaguzi Zanzibar.
Alisema ugawanyaji huo unafanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ni utekelezaji wa sheria kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Chanzo : Tanzania Daima