Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Sura ya zamani ya Zenji inapotea

$
0
0
Na Salim Said Salim
 
TOKEA nilipokuwa mdogo mpaka sasa nimekuwa nikipenda kufuga kuku, hasa kwa ajili ya kujipatia mayai na kitoweo na sio kwa biashara.
 
Nimejifunza mengi juu ya tabia ya kuku, makoo na majogoo. Kwa mfano nimegundua kuwa tembe anapotaka kutaga kwa mara ya kwanza huhangaika kama anavyokuwa mzazi anapokuwa na uchungu wa ujauzito kwa mara yake ya kwanza (mwanagenzi).
 
Miongoni mwa mafunzo niliyopata kutokana na kufuga kuku ni kile ninachoweza kukieleza kama “uungwana na ustaarabu, mila na desturi njema za kuku, tofauti na tunavyoona hii leo katika jamii ya binaadamu.
 
Sijawahi kuona na wala kusikia jogoo kumparamia kifaranga. Hata hivyo, mara nyingi nimeona jogoo akimvizia koo linalolea vifranga, lakini mara tu koo linaposimamisha mbawa na kupiga ukenje (kelele) kumtaka jogoo asimkaribie kwa vile analea, jogoo huondoka kwenda kutafuta koo jingine kutimiza kiu yake ya kimaumbile.

Mara nyingi nimekuwa nikisikitika na kushituka ninaposikia pandikizi la kijana wa miraba minne au mzee wa miaka 50 au zaidi amemhadaa au kutumia nguvu kumuingilia kitoto cha umri wa hata chini ya miaka mitatu.
Watu wengine pia wanashindwa hata na kuku wa kuwapa wazazi wenzao nafasi ya kulea na kuona uzazi wa papo kwa papo ni sahihihi.
 
Kwa maana hio kuku wanao mfumo mzuri wa uzazi wa mpangilio kuliko baadhi ya watu. Huu ndio ukweli, ijapokuwa watu wengine watanuna ninapoelezea hali hii!
 
Siku hizi katika visiwa vya Unguja na Pemba, kama ilivyo katika baadhi ya jamii za nchi za karibu na mbali, imekuwa kawaida kusikia mtu mzima anatinga mahakamani kwa kumbaka mtoto wa miaka miwili au mitatu.
 
Hivi kribuni tu mzee mmoja wa miaka 50 amefikishwa mahakamani Zanzibar kwa shitaka la kumuingilia  mbele na nyuma binti yake wa kumzaa ambaye sasa ana miaka 14.
 
Tukio kama hili huelezwa na jamii kuwa ni la kinyama, lakini kama nilivyoeleza hapo juu kuwa hata wanyama huwa na imani na viumbe wenzao wadogo.
 
Ama kweli hawakukosea baadhi ya wazee wa Zanzibar ambao husikika wakisema yanayoonekana katika visiwa vya Unguja na Pemba siku hizi ni tafauti na ilivyokuwa zamani. Masikini Zanzibar na watu wake!
 
Hata wageni waliosoma vitabu mbalimbali au kusikia habari za hali ilivyokuwa Visiwani siku za nyuma wanashangaa kuona namna Zanzibar ilivyobadilika.
 
Karibu miaka 10 iliopita, rafiki yangu mmoja aliwahi aliniambia kama patatoka miujiza ya mtu aliyekufa akajaaliwa kufufuka kuanza maisha kwa mara ya pili hatachukua muda kuiaga dunia.
 
Kifo chake kitatokana na mshituko wa moyo kwa kutoamini anayoyaona Visiwani huku akiwa amesononeka kwa kujiuliza kama hio ndio Zanzibar aliyoijua katika awamu yake ya kwanza ya kuishi Zanzibar.
 
Hapana ubishi kwamba mabadiliko ni mambo ya kawaida katika maisha ya binaadamu na hata nchi, lakini baadhi ya mabadiliko ya tabia yanayoonekana siku hizi hayakubaliki.
 
Hii ni kwa sababu ya ujahili na wenda wazimu uliopindukia mpaka na ambao hata wanyama hawaufanyi.
 
Ujahili huu unakuzwa na watu kuoneana muhali na kulindana kwa maovu na mpaka  watu watakapoacha kuvumilia ushenzi wa kudhulumu watoto, wakiwemo waliowazaa,  na kuruhusu sheria kuchukua mkondo wake.
 
Wazanzibari watajijutia kwa kufuga tabia zilizooza za kubaka watoto kama wanavyofanya kunguru na mwewe kwa vifaranga vya kuku.
 
Lakini Wazanzibari wengi sio tu wamepoteza utu wao kwa baadhi kufanya ujahili uliovuka mipaka, bali hata lugha wanayotumia siku hizi ambayo ni tafauti na zamani walipotumia mashairi yaliojaa haiba, mafumbo na methali.
 
Siku hizi matumizi ya mafumbo kama Akiba haiozi, Akipenda chongo huita kengeza, Akufukuzaye hakwambii toka, Embe mbivu yaliwa kwa uvumilivu, Tam tam Mahoinda ukila utakonda au Japo sipendezi kubembeleza siwezi hayasikiki tena katika midomo ya Wazanzibari.
 
Watu wa visiwani wametumbukia katika matumizi ya lugha iliyokosa mvuto ya maeneno kama dingi, mshikaji, msela, fulani kafulia, mikakati na matumizi ya mtusi hadharani.
 
Mafumbo yaliotoa ujumbe kwa jamii yalitumiwa kwa kuziandika kanga na kudhihirisha utajiri mkubwa wa lugha mwanana ya watu wa mwambao, hasa Zanzibar.
 
Mafumbo pia yalitumika kupeleka ujumbe wa elimu, nasaha, onyo na tahadhari kwa lugha iliyokuwa ndani ya kijaluba na kutaka aliyefungua hicho kijaluba kuchambua na kujua alichokiona au kukisikia.
 
Kwa mfano watu wa kale wa Zanzibar walisema ving’aavyo vyote sio dhahabu, kuonya ni hatari mtu kuhadaika na pambo la nje la mtu au kitu.
 
Kwa lugha nyengine ni vibaya kukihukumu kitabu kutokana na uzuri wa gamba lake. Ujumbe huu una mafunzo makubwa kwa mtu anayezingatia kauli hii.
 
Lugha mwanana  kama iliyomo kwenye mfumbo yaliyoandikwa kwenye khanga imetoweka na pole pole inageuzwa kuwa sehemu ya historia ya watu wa Vsiwani.
 
Vazi la herini lilikuwa ni kwa wanawake tu, lakini sio leo. Heshima imekuwa bidhaa adimu  na mtu kama haropoki maneno  ya ovyo na hatukani hadharani huonekana “mshamba”  kama vile shamba ni sehemu isiyofaa kuishi watu.
 
 Lakini wapo wanaosema aliopo mjini na hana asili ya shamba sio mtu wa sili ya Zanzibar bali wa kufikia.
 
Hata misikiti ambayo milango yake ilikuwa wazi saa 24, siku hizi  hukomelewa mageti ya chuma kuilinda na wizi. Siku za nyuma msikiti uliokomewa kufuli ulikuwa mmoja tu. Nao ni ule unaoitwa Msikiti Makufuli, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
 
Hii ilitokana na mbwa koko kujifungua msikitini na hapo ndio ilipoamuliwa msikiti huo uliokuwa ukitumiwa sana na wapita njia usikae wazi kama misikiti mengine.
 
Lakini leo misikiti yote Visiwani, hata ya viijini, hukomewa mchana na usiku kutokana na wizi uliokithiri wa mazulia, mabomba ya maji na hata vyoo na mishafu.
 
Majina ya mitaa ya Zanzibar nayo pia imebadilika kwa kiasi fulani. Miembe ambayo majina yake yalitawala mitaa ya Visiwani sio tu  imekatwa bali hata hayo majina yamepotea.
 
Mifano ni mitaa iliojulikana kama Mwembe Dodo, Mwembe Kidundo, Mwembe Sanda na Mwembe Kisonge. Siku hizi kumeibuka mitaa ya Magomeni, Kanyeni, Nyarugusu, Monduli, Uholanzi, Sarayevo, Bosnia, Kwa Mchina na Uholanzi.
 
Wazee wa zamani wa Visiwani walikuwa na mashindano ya kupanda miti, lakini siku hizi watu wanashindana kukata miti na hawapandi mengine mpaka ifike siku ya kampeni ya kupanda miti.
 
Baya zaidi ni kuwa  wakishaipanda hawajali kuitunza. Matokeo yake ni kuwa matunda kama fuu, pilipili doria, mbura na chongoma
yamepotea na si ajabu yakawa hayaonekani tena baada ya miaka michache.
 
Hata mavazi ya asili yanatoweka kwa haraka. Leo unaweza kuzunguka baadhi ya maeneo ya miji na vijiji na ukawahesabu wanaume waliovaa kanzu na viatu vya Makubadhi na wanawake waliovaa buibui.
 
Wanaume wanasuka nywele na kuvaa herini na wanawake wanashindana kwenda nusu uchi. Wenyewe wanasema mambo hadharani!
 
Zanzibar mpaka leo inayo sheria ya mavazi na watalii walilazimishwa kununua kanga walipofika bandarini au uwanja wa ndege ili wajistiri, lakini leo wanatembea na vichupi sokoni na mitaani na sheria zimefumbiwa macho.
 
Leo unaweza kuzunguka jua linapochomoza mpaka linapotua na hutaiona vile chakula maarufu kama manda au kinywaji murua cha togwa.Wapishi wa vyakula na vinywaji asilia wanahesabika kwa vidoke na wote sasa ni wazee.
 
Akina dada wa leo wamejikita kwa mapishi ya chipsi na mapishi ya kutumia vyungu na mkungu ambayo faida zake kiafya na kwa ladha ni makubwa yanatoweka.
 
Matumizi ya kata na upawa ni vifaa ambavyo vinaonekana katika baadhi ya vijiji na makumbusho.
 
Njia za kuhifadhi chakula kwa kufunika kawa ili kukinga wadudu na kukifanya kibakie na moto kwa muda mrefu zimeachwa.
 
Mikoba ya asili ya ukili na vikapu imewekwa pembeni na watu wamekumbatia mifuko ya plastiki ambayo inachafua mazingira.
 
Ujirani nao umetoweka. Zamani mtoto alilelewa na watu wote mtaani na mzee aliweza kumuacha mwanawe nyumba ya
jirani bila ya wasi wasi na kuangaliwa ipasavyo.
 
Leo hali ni tafauti…kila mtu anatakiwa abebe mwanawe na baadhi ya watu hawajui hata majina ya majirani zao.
 
Zamani watoto walipenda kusoma, chuoni na shule. Leo tunaambiwa wanaotoroka shule hufikia hata asilimia 30
ya darasa.
 
Ukienda kwenye fukwe za bahari unawakuta watoto wanapara samaki na wengine wanavunja kokoto au kupakia na kupakua mizigo pwani na barabarani, badala ya kusoma.
 
Siku za Sikukuu kulikuwa na michezo ya kuchekesha kwa ajili ya watoto, kama ya karagosi. Siku hizi kinachoonyeshwa ni michezo ya kuigiza ambapo utaona mwanamke anamwambia mwenzake amdanganye mume wake anakwenda matangani ili apate njia ya kwenda kufanya ufuska kwa “mshikaji wake”.
 
Siku hizi watu hungojea mikopo kutoka Mfuko wa Serikali, benki au taasisi ili kupata fedha za kufanya biashara.  Zamani watu walishirikiana na kusaidiana kwa hali na mali.
 
Watu walichangishana fedha na mmoja wao kupewa kwa zamu katika mfumo uliojulikana kama upatu. Mfumo huu ni kama wa hizi Saccos tulionazo siku hizi ambapo wengine huzitumia kutapeli wenzao.
 
Watu hawakemei maovu kama ya kondakta wa daladala kumsukuma mtoto anayebembeleza kupata usafiri wa kwenda shule au kumwambia mzee anayetumia mkongojo “Changamka” na asitokee hata mtu mmoja kumtaka asifanye hivyo kwa vile zama za mzee kama huyo kuchangamka  zimepita.
 
Zamani Zenji furaha au msiba wa familia ilikuwa ya mtaa mzima. Leo ni kawaida kusikia muziki unapigwa nyumba ya pili ambapo maiti huwa inangojea kwenda kuzikwa.
 
Wapo waliosema…chelewa chelewa utamkuta mtotosi wako na kwa hili watu wa Visiwana wasingoije mpaka wakaja kupwelewa.
 
Chanzo : Tanzania Daima

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>