Na Mwandishi wetu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeaswa kuacha kusaka umaarufu wa kisiasa kwa kuuchupia mjadala wa kidiplomasia kati ya Rais Jakaya Kikwete na Rais Paul Kagame wa Rwanda.Tahadhari hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Makatibu wa itikadi na uenezi 80 katika mkutano uliofanyika Vitongoji Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema uamuzi wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa kuingilia kwake mvutano huo na kumuunga mkono Rais Kagame ambaye anapinga ushauri sahihi uliotolewa na Rais Kikwete na kutoa maneno ya kejeli na jeuri kimemvunjia hadhi na kumpotezea staha mbele ya Watanzania.
Alisema Chadema hakitaweza kuyafikia malengo yao kisiasa na ndoto ya kushika madaraka kwa kutoa matamshi yasioheshimu umoja na kwa kujifanya watetezi wa uovu katika mambo ya nyeti hasa ya kimataifa na kidiplomasia.
"Dk. Slaa aheshimu utu uzima wake,atumie busara, maarifa na uzoefu wake,aweke pembeni siasa za mitaani, uzalendo na utaifa, kwanza siasa za ndani zije baadae,” alisema.
Alisema ikiwa jambo hilo litahatarisha mahusiano na maelewano si chama chake wala CCM itakayofaidika bali wananchi wa pande mbili ndiyo watakaopata matatizo.
Aliwataka viongozi wa Chadema kujali msingi wa umoja, ushirikiano na mashirikiano kuliko kusaka umaarufu unaokiuka taratibu zinazoweza kuathiri mahusiano mema.
"Ndugu ni ndugu yako daima, rafiki mwema ni ndugu wa mwenzako, Chadema isiache mbachao kwa msala upitao, tutavutana kisiasa ila hatutagawanyika,”aliongeza.
Aliwataka Makatibu wa siasa na uenezi wa CCM ngazi za mikoa,wilaya, majimbo na wadi kujifunza na kupata ufahamu wa kutosha juu ya matumizi ya teknolojia ya mwasiliano na habari.