Na Mwandishi wetu
BARAZA la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limeunga mkono kauli ya Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu kwa kuitaka serikali kuchunguza kwa kina tukio lililopelekea kupigwa risasasi kwa mhubiri wa kiislamu, Sheikh Issa Ponda. Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Al Had Musa Salum alisema ingawa BAKWATA limekuwa likipingana na misimamo ya Sheikh Ponda, lakini serikali ilikuwa na nafasi ya kumkamata Ponda kwa kufuata mkondo wa sheria.
Sheikh huyo ambaye amekuwa katika mivutano ya mara kwa mara na serikali alidaiwa kupipigwa risasi baada ya kutokea vurugu mjini Morogoro.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Taasisi za Kisilamu,Mussa Kundecha, alisema endapo serikali haitachukua hatua itakayowaridhisha Waislamu, wataamua kufikiria upya mustakabali wao na serikali ya Tanzania.
Sheikh Ponda amelazwa katika hospitali ya taifa, Muhimbili, mjini Dar es Salaam akiuguza jeraha linalodaiwa kuwa la risasi huku akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu.
Msemaji wa Jeshi la polisi, Advera Senso amesema polisi kwa kushirikiana na jukwaa la haki jinai wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo huku akikana kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi na polisi.
Senso aliwalaumu wafuasi wa Sheikh Ponda kwa kuwazuia askari kumkamata baada ya kuwarushia mawe; hatua iliyosababisha askari hao kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya na hata hivyo wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha kiongozi huyo.
Taarifa za jumuiya hiyo ambayo inajulikana zaidi kama Shura ya Maimamu zinasema Sheikh Ponda ambaye polisi wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za kutoa matamko ya uchochezi, alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi Dar es Salaam zaidi ya kilomita 200.
Sheikh Ponda kwa sasa anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja alichohukumiwa mapema mwaka huu baada ya kukutwa na makosa kadhaa ikiwemo uchochezi wa kuharibu mali za watu.