· Afafanua kuhusu Gharama za Serikali Tatu
Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba amewataka watu wenye ulemavu kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya katiba ili kuiwezesha Tume yake kujua mahitaji yao na kuyafanyia kazi.
Akizungumza katika siku ya kwanza ya mkutano wa Baraza Maalum la Katiba kwa ajili ya watu wenye ulemavu mjini Dodoma leo (Alhamisi, Agosti 15, 2013), Jaji Warioba amesema Tume yake inatarajia kupata maoni mazuri yanayohusu watu wenye ulemavu kutoka katika baraza hilo.
“Mtusaidie kupata maoni kuhusu maeneo yote ya rasimu ya katiba yanayohusu watu wenye ulemavu,” alisema na kuongeza kuwa hilo lisiwazuie kutoa maoni kuhusu maeneo mengine ya rasimu ya katiba.
“Nyie pia ni sehemu watanzania na hata mkiwa viongozi mtakuwa viongozi wa watanzania wote... kwa hiyo ipitieni rasimu yote na mtoe maoni katika maeneo yote pia,” alisisitiza Jaji Warioba na kuongeza kuwa Tume yake pia iliandaa Baraza Maalum kama hilo Zanzibar kwa kushirikiana na Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ).
Akiongea katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Shirikisho la Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Bw. Novatus Rukwago aliishukuru Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuwezesha kufanyika kwa baraza hilo na kusema kuwa mkutano huo umeshirikisha vyama vyote kumi vya watu wenye ulemavu.
Alivitaja vyama hivyo kuwa ni Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo (CHAWATA), Chama cha Wasiiona (TLB), Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Afya ya Akili (TUSPO) na Chama cha Watu Wenye Ulemavu Walioumia Uti wa Mgongo Kilimanjaro (KASI).
Vyama vingine vinavyohudhuria mkutano huo ni Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Mabaka ya Ngozi (PSORATA), Chama cha Albino Tanzania (CAT), Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Akili (TAMH), Chama cha Viziwi Wasioona (TASODEB) na Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Vichwa Vikubwa na Mgongo Wazi (ASBAHT).
Kuhusu Gharama za Muungano
Katika hatua nyingine, Jaji Warioba amefafanua kuhusu gharama za uendeshaji wa muungano wa shirikisho la Serikali tatu ambao umependekezwa na Tume yake katika rasimu ya katiba iliyozinduliwa Juni 3 mwaka huu.
Akijibu swali la mjumbe mmoja wa Baraza hilo aliyeomba ufafanuzi kuhusu gharama za uendeshaji wa Serikali ya Muungano ndani ya shirikisho, Jaji Warioba amesema Tume yake imependekeza Serikali ya Muungano iendeshwe na mapato yatakayotokana na ushuru wa bidhaa ambao unakua kila mwaka.
“Tumependekeza chanzo hiki kikubwa cha ushuru wa bidhaa baada ya kupokea maoni ya wataalam na kujiridhisha,” alisema na kufafanua kuwa mapato yanayotokana na ushuru wa bidhaa yanatosha kuendesha shughuli za Serikali ya Muungano inayopendekezwa.
Akiongea kuhusu suala hilo katika mkutano huo, Mjumbe mwingine wa Tume hiyo Bw. Ally Saleh amesema kwa sasa mapato ya ushuru wa bidhaa ni zaidi shilingi trilioni moja na kuwa maoni ya wataalam ambayo Tume yake imeyapokea yanaonyesha kuwa kwa kiasi kikubwa mapato hayo yanakua kila mwaka.
“Kwa hiyo mapato haya ya ushuru wa bidhaa yanatosha kuifanya Serikali ya Muungano ijisimamie na mapato mengine waachiwe washirika wa Muungano,” amesema.
Mkutano huo wa Baraza Maalum la Watu Wenye Ulemavu unamalizika kesho (Alhamisi, Agosti 16, 2013). Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaendelea na mikutano ya Mabaraza ya Katiba ili kupokea maoni kuhusu rasimu ya katiba. Mikutano hiyo inatarajia kumalizika Septemba 2 mwaka huu.