Na Benedict Liwenga, Maelezo
UMOJA wa Machifu Tanzania (UMT), umewasilisha nyongeza ya mapendekezo yake kuhusu katiba mpya kwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,Samia Suluhu Hassan.
Akiuwakilisha umoja huo, Chifu kutoka Magu, John Nyanza, alimueleza Samia kwamba wanaishauri serikali kutayarisha mkakati wa kitaifa wa utamaduni ili mpango mkakati huo uwe dira ya utamaduni.
Naye Chifu kutoka Ntuzu Bariadi, Agnes Ndaturu, alisema mapendekezo yao yatasaidia kuwatambua waganga wa jadi pamoja na mipaka ya kazi zao.
“Mapendekezo haya yatasaidia viongozi wa waganga wa jadi nchini kuwatambua wale waganga wanaokiuka maadili ya shughuli zao mfano mauaji ya albino, kwa kuwa kila kiongozi atakuwa anawatambua waganga wa eneo lake,” alisema Chifu Ndaturu.
Alisema wajumbe wenzao waliowatuma kuwawakilisha wanasisitiza juu ya umuhimu wa utamaduni kupewa nafasi rasmi katika katiba mpya na serikali ili pawepo kipaumbele katika utekelezaji wake nchini.
Wakizungumza kwa kauli moja, walisema suala la utamaduni katika rasimu ya pili ya katiba lifanyiwe marekebisho kwa kuzingatia mapendekezo yaliyobainishwa huku msisitizo wao ukiwa katiba kueleza wazi sera na sheria mpya zitakazotungwa zihakikishe Tume ya taifa ya utamaduni inaanzishwa.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samia Suluhu Hassan, aliwatotoa wasiwasi wawakilishi wa umoja huo kwamba atayawasilisha katika Kamati ya Uongozi ya Bunge.