Na James Gashumba
SERIKALI ya Tanzania imetangaza mipango mipya itakayorahisisha upakuaji wa mazigo katika bandari ya Dar es Salaam.
Waziri wa Uchukuzi wa Tanzania, Dk. Harison Mwakyembe, alisema mipango iko mbioni ya kukarabati maeneo ya kupakulia mizigo kutoka moja hadi saba na kujenga maeneo mengine mapya manne ya aina hiyo ili kurahisisha upakuajia wa mizigo.
Alikuwa anazungumza katika mkutano wa wakala wa usafirishaji mizigo (CCTTFA) uliokuwa unafanyika mjini Kigali, Rwanda mwishoni mwa wiki.
Alisema mamlaka ya bandari hiyo pia imetenga eneo lililo karibu na bandari hiyo kwa lengo la kujenga bandari ya nchi kavu ili kuhudumia shehena zinazosafrishwa kwenda katika nchi za Rwanda, Burundi,Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Takwimu zinaonesha kwamba asilimia 50 ya shehena zinasosafirishwa ndani na nje ya Rwanda zinapitia bandari ya Dar es Salaam.
Alisema kwamba kutokana na juhudi hizo mpya idadi ya siku za kusafirisha shehena kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda Rusumo, mpakani mwa Rwanda na Tanzania zitapungua kutoka siku 3.5 hadi 2.5.
“Tunahitaji mwingiliano zaidi, baina ya wadau wote na serikali zetu,” alisema.
Wasafirishaji mizigo awali walilalamika juu ya kuwepo kwa urasimu,rushwa na wizi katika bandari ya Dar es Salaam, mambo ambayo mpango huo mpya unakabiliana nayo kuyadhibiti.
Makamu wa Rais wa Chama cha Madereva wa Magari Yaendayo Safari Ndefu nchini Rwanda (ACPLRWA), Issa Mugarura, alisema wamekuwa wakihakikishiwa huduma hiyo na serikali ya Tanzania wakati wote lakini utekelezaji bado ni changamoto.
Hivi sasa bandari ya Dar es Salaam inapokea shehena ya tani 13.5 milioni kwa mwaka na inatarajiwa kuongezeka na kufikia tani 18 milioni baada ya kukamilika kwa mabadiliko hayo mapya.