STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 29 Agosti , 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein anaondoka nchini leo kwenda visiwa vya Samoa kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Nchi za Visiwa.
Kaulimbiu ya mkutano huo wa siku nne unaoanza Jumatatu ijayo tarehe 01 Septemba na kumalizika tarehe 04 Septemba, 2014 ni maendeleo endelevu kwa nchi za visiwa kupitia ushirikiano wa kweli.
Katika mkutano huo washiriki watajadili mada mbalimbali na namna ya kuimarisha ushirikiano katika masuala ya maendeleo endelevu ikiwemo masuala ya mazingira kama vile mabadiliko ya tabia nchi na kukabiliana na majaga, bayoanuai, maji na usafi wa mazingira na usalama wa chakula.
Masuala mengine ni afya, nishati, vijana na wanawake pamoja na mjadala ya namna sekta binafsi inavyoweza kushiriki katika kutimiza azma ya kuleta maendeleo endelevu katika nchi za visiwa.
Sambamba na kuhudhuria mkutano huo, Dk. Shein atashiriki uzinduzi wa Mpango wa Magharibi ya Bahari ya Hindi wa Changamoto za Ukanda wa Pwani na Mabadiliko ya Tabianchi (Western Indian Ocean Coastal Challenges-WIO-CC).
Chini ya mpango huo ambao unaoshirikisha visiwa vya Sycheles, Comoros, Mauirtius, Madagascar, Reunion na Zanzibar kwa pamoja visiwa hivyo vinashirikiana katika kusimamia mipango mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu ya visiwa hivyo.
Miongoni wa wajumbe wa msafara wa Mheshimiwa Rais ni pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dk. Mahadhi Juma Maalim, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Fatma Abdulhabib Fereji, Naibu Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Ramadhani Muombwa Miwnyi na Mshauri wa Rais Masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Uchumi na Uwekezaji Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anatarajiwa kurejea nchi tarehe 6 Septemba, 2014
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822