Na Kauthar Abdalla
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Mhe. Said Ali Mbarouk, ameasa kwamba mitizamo ya kisiasa na kiitikadi isipewe nafasi katika uendeshaji wa shughuli za jumuiya.
Alisema uzoefu unaonesha shughuli za kisiasa zikitawala, msukumo wa maendeleo huvia na ndio chanzo cha kusambaratika kwa jumuiya nyingi.
Alieleza hayo katika uzinduzi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Watu wa Junguni (JUMJU) uliofanyika hoteli ya Bwawani.
Alisema jumuiya zenye kusukuma maendeleo zina faida kwa jamii na serikali na ndio kichochoe cha kuleta maendeleo.
Alisema kuna jumuiya nyingi zilizoanzishwa lakini zimeshindwa kufikia malengo kutokana na wanajumuiya kutokwa na umoja wakati wa utekelezaji.
Alisema anaamini jumuiya hiyo itaongeza kasi ya maendeleo katika kijiji hichi kilichomo ndani ya jimbo la Gando.
Katibu wa jumuiya hiyo, Sada Khamis Juma, alisema lengo la kuundwa jumuiya hiyo ni kuunganisha nguvu za watu wa kijiji cha Junguni walioko nje ya kijiji hicho ili kutatua changamoto zinazowakabili watoto na ndugu zao.
Alisema moja ya changamoto inayowakabili wakazi wa kijiji hicho ni ni kutokuwepo walimu wa kutosha, maabara, maktaba na kompyuta.