STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar Jumatano 03 Septemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Apia, Samoa
Kituo cha Kimataifa cha Biashara (ITC) kimesema kiko tayari kuisaidia Zanzibar kutekeleza mkakati wake wa kuongeza ajira kwa vijana na kinamama kwa kutumia rasilimali zilizopo Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho chenye makao yake makuu mjini Geneva Uswizi, Bibi Arancha Gonzalez alieleza hayo jana wakati alipokutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein mjini hapa.
Bibi Gonzalez alibainisha kuwa kisiwa kama Zanzibar ambacho hakina rasilimali kubwa ya ardhi mauzo ya mazao yake ya kilimo hayana budi kufanyika yakiwa yameongezwa thamani.
“suala muhimu la kuzingatia ni namna gani nchi za visiwa kama Zanzibar zin
aweza kupata maendeleo kwa kutumia rasilimali zake zenyewe iwe ni kilimo au utalii” alieleza Bibi Gonzalez.
Kwa hivyo alimueleza Mheshimiwa Rais kuwa suala kubwa la kuzingatia kwa Zanzibar ni kuongeza thamani ya mazao yake kama viungo kwa kuongeza ubora na kuvipa hadhi ya pekee (branding).
Kwa upande mwingine alieleza kuwa azma ya taasisi yake ni kusaidia kuimarisha miradi midogomidogo na ya ngazi ya kati ya vijana na wanawake hivyo kuongeza ajira ili kupunguza tatizo la ajira na umasikini katika jamii.
Mkurugenzi Mtendaji huyo alimueleza Mheshimiwa Rais kuwa Taasisi yake itashirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhakikisha kuwa inakuwa na mpango utakaowahusisha vijana wengi katika sekta ya utalii kwa maana ya ajira na kubuni shughuli zinazohusiana na sekta hiyo.
“Ni sekta yenye uwezo wa kutoa ajira nyingi...jambo la lazima hapa ni kubuni shughuli ambazo zitawafanya vijana wengi kuwa sehemu ya sekta hii iwe kama waajiriwa kwa upande mmoja na upande wamejiajiri kwenye shughuli zinazohusiana na sekta hii” alisisitiza.
Katika mnasaba huo Bibi Gonzalez alieleza umuhimu wa Serikali kuhakikisha kuwa mitaala ya elimu inazingatia mahitaji ya soko la ajira pamoja na uwezo wa wahitimu kujiajiri wenyewe.
Akijibu maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji huyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alimueleza Bibi Gonzalez kuwa anakubaliana na hoja ya kuiunganisha sekta ya utalii na jamii ili iweze kutoa matokeo mazuri zaidi ikiwemo kutoa ajira nyingi kwa vijana.
“Nakubaliana na maelezo yako na Serikali imeliwekea suala hilo mkakati maalum na ndio maana tumeanzisha mpango wa Utalii kwa Wote ambao lengo lake ni kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu katika kukuza utalii na inafaidika nao” Dk. Shein alifafanua.
Kwa hivyo alisema Serikali inaipokea kwa mikono miwili dhamira ya Taasisi hiyo ya kushirikiana na nayo katika kutekeleza mpango huo ambao inaamini kuwa ni ufunguo katika kupunguza tatizo la ajira nchini.
Alimueleza Bibi Gonzalez kuwa Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuwawezeha vijana na kinamama kujiajiri kutokana na uwezo mdogo wa serikali kumpatia ajira kila mhitimu.
Alizitaja jitihada hizo kuwa ni pamoja na kanzisha mfuko wa uwekezaji pamoja na kuandaa mpango wa kuwapatia wajasiriamali dhamana za kibenki ili kupata mitaji.
“Ni dhahiri kuwa Serikali hatuwezi kumpatia ajira kila mhitimu ambapo kwa sasa tuna wahitimu wa ngazi mbalimbali kuanzia skuli za sekondari hadi vyuo vikuu” Alieleza Dk. Shein.
Hata hivyo alimueleza Mkurugenzi Mtendaji huyo kuwa inatia moyo kuona vijana wengi na kinamama wanajishughulisha na kazi za uzalishaji wa bidhaa na zaidi wanaziongeza thamani.
“tumeshuhudia vijana wengi katika miaka ya karibuni wakiwa katika vikundi wakianzisha biashara na kuzifunga zikiwa zimeongezwa thamani na kujitambulisha kwa wateja kupitia maonesho mbalimbali ya biashara” alieleza Dk. Shein.
Aliongeza kuwa pamoja na mwitikio huo kumejitokeza changamoto nyingine ya wajasiriamali wengi kuzalisha bidhaa zinazofanana kunakosababisha bidhaa kufurika katika masoko na hata wakati mwingine kuathiri mwenendo wa biashara zao.
Katika mazungumzo hayo ambayo yalifanyika sambamba na Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa Nchi za Visiwa unaoendelea hapa, Dk. Shein aliishukuru Taasisi ya Kimataifa ya Biashara kwa msaada wake katika kuzifanya karafuu za Zanzibar kuwa na sifa za pekee(Branding).
Alimueleza Mkurugenzi huyo kuwa jitihada za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuimarisha zao la karafuu zimeanza kuzaa matunda ambapo wakulima wamehamasika na sasa wanathamini na kukipa uzito kilimo hicho hatua ambayo imesababisha uzalishaji wa zao hilo kuongezeka.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822