Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein : China ni marafiki wa kweli

$
0
0
Na Said Ameir, ikulu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuongezeka nchini kwa misaada ya ushirikiano kutoka Jamhuri ya Watu wa China ni kielelezo thabiti cha uimara wa uhusiano wa kidugu na ushirikiano wa kihistoria kati ya Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
 
Rais ametoa kauli hiyo  wakati alipokuwa akizungumza na Balozi mdogo wa China nchini Bibi Chen Qiman ambaye alifika Ikulu leo kumuaga Rais kufuatia kumalizika kwa kipindi cha utumishi wake nchini.
 
“Tumeshuhudia miradi mingi ikianzishwa na kutekelezwa katika kipindi chako cha kuitumikia nchi yako hapa Zanzibar na hii ni faraja kwa Serikali na wananchi wa Zanzibar” alieleza Dk. Shein.
 
Dk. Shein amemueleza Bibi Qiman kuwa misaada ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China katika sekta mbalimbali kama afya, usafirishaji na uimarishaji rasilimali watu imesaidia kuimarisha uwezo wa Serikali wa kutoa huduma kwa wananchi.
 
“Nimeguswa sana na msaada wenu katika kuimarisha rasilimali watu katika Serikali na taasisi zake ambapo watumishi wa ngazi  mbalimbali wamefaidika na fursa za mafunzo yanayotolewa na Serikali yenu” Alieleza Dk. Shein na kuongeza kuwa huo ni msaada mkubwa mbao utaleta manufaa mengi kwa Zanzibar hivi sasa na kwa baadae.
 
Alimshukuru Bibi Qiman kwa utumishi wake bora wakati wote akiwa Zanzibar na kueleza kuwa amekuwa chachu ya misaada  ambayo Zanzibar imekuwa ikiipata kutoka Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
 
Katika mazungumzo hayo Rais wa Zanzibar alisisitiza tena dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi wake ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Watu wa China.
 
“Ningependa kukuhakikishia tena kuwa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Wananchi wake ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wetu na Serikali na wananchi wa China ni thabiti kwa kuwa nyinyi ni washirika wetu na ni ndugu zetu” alieleza Dk. Shein.
 
Rais ametoa rai ya kuendelezwa kwa utaratibu wa kutembeleana kati ya Zanzibar na China ikiwa ni njia mojawapo muhimu ya kuimairsha uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo.
 
Kwa hiyo Dk. Shein amemueleza bibi Qiman kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na wananchi kwa jumla wana matumaini makubwa katika ushiriki wake kwenye utekelezaji wa Mpango wa Ushirikiano kati ya Afrika na China.
 
Serikali, alisema Dk. Shein, itampa ushirikiano Balozi mpya atakayechukua nafasi ya Bibi Qiman kama ilivyokuwa kwake ili aweze kutimiza majukumu yake ya kuendeleza na kuimarisha uhusiano kati ya Zanzibar na China.
Wakati huo huo Balozi mdogo wa China anayemaliza muda wake Bibi Chen Qiman amesema katika kipindi cha miaka miwili na nusu ya utumishi wake nchini ameshuhudia mabadiliko makubwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
 
“Nimeshuhudia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika nyanja mbalimbali katika kipindi cha utumishi wangu hapa na hii ni uthibitisho kuwa Zanzibar iko katika mwelekeo mzuri kimaendeleo na kwamba inasonga mbele” alisema Bibi Qiman.
 
Amemueleza Rais kuwa anaondoka Zanzibar akiwa na kumbukumbu nzuri ya utumishi wake ambao alisema umekuwa bora na kuushukuru uongozi wa Serikali na wananchi wa Zanzibar kwa ushirikiano ambao umemfanya aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
 
“Tumeshirikiana kwa karibu wakati wote na tumeshuhudia miradi mingi ikitekelezwa katika nyanja mbalimbali na naamini majukumu yangu nimeyatekeleza vizuri” alieleza Bibi Qiman.
Bibi Qiman aliahidi kuwa balozi mzuri wa Zanzibar huko anakokwenda na kusema kuwa hatasita kuueleza ulimwengu sifa za Zanzibar na watu wake.
 
“Nitakuwa balozi mzuri wa Zanzibar nitaeleza sifa zake kuwa ni kisiwa chenye mandhari nzuri na ya kupendeza. Ni kisiwa cha amani na utulivu chenye watu wakarimu na wastarabu” alisema na kuongeza kuwa wananchi wengi wa China walioishi na kufanyakzi Zanzibar bado wana hamu kurejea kutokana na kumbukumbu nzuri ya maisha waliyoishi hapa.
 
Bibi Qiman alisema anatarajia kuona uwekezaji zaidi kutoka nchini China katika visiwa vya Unguja na Pemba na kwamba ziara ya Rais wa Zanzibar  aliyoifanya nchini China hivi karibuni imeleta msukumo mkubwa katika kupanua maeneo ya ushirikiano kati ya nchi mbili hizo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>