Na Mwashamba Juma
WAFANYAKAZI wa Shirika la Magazeti ya Serikali, linalochapisha magazeti ya Zanzibar Leo, Zanzibar Leo Jumapili na Zaspoti, wameaswa kujenga ushirikiano na udugu katika kufanikisha majukumu ya kazi zao.
Wito huo ulitolewa jana na Mhariri Mtendaji wa Shirika hilo, Abdulla Mohammed Juma, katika mkutano wa wafanyakazi wa shirika hilo.
Alisema umoja na ushirikiano hautopatikana katika maeneo ya kazi zao ikiwa wafanyakazi hawatothaminiana na kuheshimiana kwenye utendaji wa kazi zao sambamba na kuwataka kila mmoja kuheshimu kazi ya mwengine kwani kila kazi ina ugumu wake.
Akizungumzia baadhi ya changamoto kwa idara za shirika hilo, aliwataka wakuu wa idara kufanya maamuzi kisheria wanapotatua mizozo ya wafanyakazi wao badala ya kusikiliza malalamiko ya upande mmoja.
“Kabla ya kufanya maamuzi ya malalamiko ya wafanyakazi wetu, ni lazima tufanye mawasiliano nao ili tuamue kisheria,” alifahamisha.
Nae Naibu Mhariri Mtendaji wa Shirika hilo, Nasima Haji Chum, aliwaomba wafanyakazi kuepuka majungu badala yake kufanyakazi kwa ushirikiano.
Aidha aliwataka kuepuka makundi yenye lengo la kuweka ubaguzi baina yao.
Kwa upande wao wafanyakazi waliwaomba viongozi wao kuimarisha mawasiliano baina yao ili kuepusha migogoro ambayo ni chanzo cha kurudisha nyuma maendeleo ya shirika hilo.
Waliwataka wakuu wa idara kuepuka upendeleo baina ya wafanyakazi ili kuondosha matabaka, chuki na uhasama.