Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Mahakama Kuu yampa nafasi ya mwisho DPP Akishindwa kukamilisha ushahidi kesi itafutwa

$
0
0
Na Khamis Amani
IKIWA ni mwaka mmoja, miezi minne na siku 19 zimepita, tokea kuuawa kwa Padri Evaristus Gabriel Mushi na upelelezi wake ukiwa bado haujakamilika, Mahakama Kuu ya Zanzibar imetoa muda wa mwisho wa kuendelea na kesi hiyo.

Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, ambae ndie anaesikiliza kesi hiyo, alisema Oktoba 3 mwaka huu ataiondoa kesi hiyo mahakamani ikiwa upande wa mashitaka utashindwa kukamilisha upelelezi huo.

Uamuzi huo wa mahakama umekuja baada ya kesi hiyo inayomkabili Omar Mussa Makame (35) kukaa kwa muda mrefu bila ya kusikilizwa, huku upande wa mashitaka ukiomba muda zaidi wa kukamilisha upelelezi huo ombi ambalo lilipingwa na upande wa utetezi.

Upande wa utetezi ulioongozwa na Wakili wa kujitegemea Abdallah Juma Mohammed wa kampuni ya AJM Soliciter & Advocate Chamber, aliiambia mahakama hiyo kuchoshwa na nyimbo za mara kwa mara za upande wa mashitaka juu ya upelelezi wa kesi hiyo ambapo kila kesi hiyo inapoitwa mahakamani upande huo unadai haujakamilika.

Alidai, madai ya upande wa mashitaka ya kuwa upelelezi wa kesi hiyo  haujakamilika hayana msingi wowote, ukizingatia kesi hiyo ni ya muda mrefu.


Hivyo, wakili huyo aliiomba mahakama imwachilie huru mteja wake bila masharti yoyote na upande wa mashitaka ukijipanga unaweza kuirudisha tena mahakamani kesi hiyo kwa mujibu wa taratibu za kisheria.

“Mheshimiwa jinai haiozi, wanaweza wakaileta tena mahakamani wakati wowote baada ya kujipanga, kuachiliwa huru kwa mteja wangu haina maana kama haitafunguliwa tena kesi hii”, alifahamisha Wakili huyo.

Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Abdallah Mgongo licha ya kukiri kwamba kesi hiyo ni ya muda mrefu,aliiomba mahakama kuangalia uzito wa kesi hiyo ili kuona haki inatendeka.

Alidai kuiahirishwa kwa ajili ya kuendelea na upelelezi wa kesi hiyo ni sababu ya msingi kwa upande wao,hivyo aliiomba mahakama kuipangia tarehe nyengine ya kutajwa ili kuendelea na upelelezi huo.

Aliai upande wa mashitaka una jukumu la kusimamia mwenendo wa kesi mahakamani na suala la upelelezi lipo chini ya mikono ya polisi kwa mujibu wa kifungu cha 74 (1) cha sheria za mwenendo wa jinai (CPA) namba 7/2004 sheria za Zanzibar.

“Ni kweli hili shitaka ni  la muda mrefu kwa hesabu za haraka haraka limeahirishwa mara 22, hatuwezi kusema ni lini upelelezi wake utakamilika,” alidai.

Hoja hizo zilipingwa na Wakili wa utetezi kwa madai shitaka hilo halistahiki kuwepo mahakamani, kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kukiri lini suala la upelelezi litakwisha na ni uthibitisho tosha kuwa kesi hiyo itaendelea kufikishwa mahakamani na kumpotezea muda mteja wake.

Baada ya kusikiliza hoja za pande mbili hizo, Jaji Omar Othman Makungu alikiri kuwa ni shitaka la muda mrefu lakini si busara kuondoshwa mahakamani kwa kushitukiza bali inapaswa kutolewa muda wa ziada kwa upande wa mashitaka ili kujipanga zaidi.

Hivyo aliupa muda wa mwisho upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi huo na endapo katika kikao kijacho utashindwa, mahakama italiondosha shauri hilo.

Kesi hiyo ilifunguliwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Aprili 5 mwaka jana, ambapo mshitakiwa huyo alisomewa shitaka la kuua kwa makusudi kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya kanuni ya adhabu sheria namba 6/2004 sheria za Zanzibar.


Siku hiyo mshitakiwa huyo akiwa mbele ya Mrajis wa Mahakama Kuu George Joseph Kazi, alidaiwa kumuua kwa makusudi Evaristus Mushi tukio lililodaiwa kutokea Beit el ras wilaya ya magharibi Unguja, majira ya saa 12:50 za asubuhi ya Februari 17 mwaka jana.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>