Na Amina Omari,Tanga
Madiwani wa CUF wilayani Tanga, wamesababisha kuahirishwa kwa muda wa zaidi ya saa tatu kikao cha kamati ya fedha na uchumi wakipinga mjumbe mwengine, Mohamed Mambea, kushiriki kikao hicho kwa madai si mjumbe halali.
Diwani huyo alikihama chama hicho hivi karibuni na kujiunga na CCM.
Hali hiyo ilimlazimu Mstahiki Meya wa jiji la Tanga, Omari Guled, kuahirisha kwa muda kikoa hicho ili kutoa fursa ya kusikiliza hoja zao.
Kikao hicho cha kamati kilikuwa kinajadili hoja zilizotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya kuwasilisha kwenye kikoa cha Mkuu wa Mkoa, Chiku Gallawa hivi karibuni.
Akizungumza na gazeti hilo, Naibu Meya Muzamil Shemdoe, alisema kitendo kilichofanywa na Madiwani WA CUF ni uhuni na ni tukio la kusikitisha kwani badala ya kufuata taratibu wao walivamia mkutano.
“Hawa wamefanya uhuni, sheria ipo na taratibu zipo za kufuata ili sherai iweze kufanya kazi ipasavyo sasa wao badala ya kufuata utaratibu wa kimaandishi wao wanakurupuka na kuja kutuharibia kikao chetu,” alisema.
Alisema kikao kilianza majira ya saa nne asubuhi na baada ya kama nusu saa ndipo wadiwani hao kama saba walipovamia kikoa hicho na kumtaka Mambea atokee kwenye kamati hiyo kwani sio mjumbe halali na hana haki ya kushiriki.
Hata hivyo madiwani hao wakiongozwa na Diwani wa kata ya Ngamiani Kusini, Mussa Mbaruku, walilazimika kwenda ofisi za Mkurungenzi wa jiji, Juliana Malange, kuelekezwa taratibu za kufuata.