Na Masanja Mabula,Pemba
Vitambulisho 13,698 vya Mzanzibari Mkaazi kutoka wilaya nne za Pemba, vimerejeshwa ofisi kuu Unguja, baada ya kumaliza muda wake wa matumizi vikiwa katika ofisi za Pemba bila ya kuchukuliwa wa wahusika.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Ofisa wa Vitambulisho vya Mzanzibar Pemba, Hamad Shamata Hamad, alisema kati ya vitambulisho hivyo 7,369 vinatoka mkoa wa kusini Pemba.
Alisema ofisi ya vitambulisho imefikia uamuzi wa kuvirejesha ofisi kuu baada ya kukaa kwa muda mrefu na wenyewe hawakujitokeza kuvichukua.
Alisema wilaya ya Chake Cheke ndio inayoongoza kwa kuwa na vitambulisho vingi ikilinganishwa na wilaya nyingine ambayo ilikuwa na vitambulisho 4,238 ikifuatiwa na wilaya ya Mkoani iliyokuwa na vitambulisho 3,131.
Aidha alisema kuwa katika wilaya ya Wete jumla ya vitambulisho 3,208 vimerejeshwa wakati vitambulisho 3,121 vimerejeshwa kutoka wilaya ya Micheweni.
Akitoa uchambuzi kimajimbo , Shamata alisema jimbo la Wawi ndio kinara likiwa na vitambulisho 1,349 likifuatiwa na jimbo la Chake Chake (1,079) na jimbo la Ziwani (1,004).
Kwa upande wa wilaya ya Micheweni,jimbo la Konde ndilo linaloongoza kwa kuwa na vitambulisho 922 wakati jimbo la Mkoani linaongoza kwa wilaya ya Mkoani kwa kuwa na vitambulisho 790 ambapo kwa wilaya ya Wete, jimbo la Wete linajumla ya vitambulisho 963.
Alisema wananchi ambao vitambulisho vyao vimerejeshwa wakihitaji vitambulisho wanatakiwa kuanza taratibu upya ikiwa ni pamoja na kuomba fomu kwa sheha wa shehia husika.