Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein aungana na wananchi katika maziko ya aliyekuwa Spika mstaafu wa BLW

$
0
0
STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

    Zanzibar                                                                                       04 Septemba , 2014
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein leo ameongoza mazishi ya marehemu Mhe. Ali Khamis Abdalla aliyekuwa Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

 
Mazishi ya Marehemu Ali Khamis Abdalla yalifanyika Fuoni, Wilaya ya Magharibi Unguja Mkoa wa Mjini Magharibi, ambapo miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Pandu Ameir Kificho.

 
Wengine ni Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, viongozi wengine wa dini, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wakuu wa vikosi vya Ulinzi na Usalama pmoja na viongozi wengine vyama vya siasa na Serikali.

 
Mapema Dk. Shein alishiriki na kuungana na wananchi pamoja na wanafamilia na viongozi mbali mbali wa dini vyama na Serikali katika sala  ya kumsalia Marehemu Ali Khamis Abdalla iliyofanyika huko katika Mskiti wa Masjid Mahfoudh-Mazizini nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

 
Mazishi hayo yalifanyika kwa heshima zote za Kidini na Serikali ikiwa ni pamoja na kupigwa risasi baridi pamoja na Paredi la Jeshi la Polisi.

 
Mheshimiwa Ali Kahmis Abdalla alizaliwa mwaka 1914 Nganani, Makunduchi na alikulia katika kijiji cha Ndijani na kupata elimu yake ya awali mwaka 1925 katika skuli ya Ndijani hadi mwaka 1928.

 Akisoma wasifu wa marehemu katika mazishi hayo, Mkuu wa Utawala wa Baraza la Wawakilishi Amour Mohamed Amour alieleza kuwa  baada ya kufaulu mitihani ya skuli ya msingi mnamo mwaka 1929 alijiunga na Skuli ya Ben bella (Government Boys School) hadi mwaka 1932 na baadae katika mwaka 1933 aliendelea na mafunzo ya Ualimu katika skuli hiyo hiyo ya Benbella na kutunukiwa cheti cha Ualamu.

 Marehemu alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda kwenye mwaka 1935-1941, katika fani ya Stashahada ya Kilimo.

Baada ya kurejea masomoni aliajiriwa kama Msaidizi Afisa Kilimo (Assistance Agricultural Oficer) mnamo mwaka 1942 ambapo mnamo mwaka 1952 aliteuliwa kuwa Meneja wa shamba la Serikali Kizimbani, pamoja na majukumu hayo aliendelea na kazi hizo za kilimo  katika maeneo ya Chukwani na Selemu Pemba hadi mwaka 1963.
 
Mwisho wa mwaka wa 1963 alichaguliwa kuwa Katibu katika Ubalozi wa Zanzibar nchini Misri na alitumikia kwa miezi minne hadi April 1964, baadae aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo hadi 1967 na mwaka 1968-1975 alifanya kazi katika mashamba ya Mikonge  huko Tanga.
 
Mnamo tarehe 21 Oktoba mwaka 1985 alichaguliwa kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi akiwa Spika wa Pili toka kuanzishwa kwa Baraza hilo mwaka 1980 na alidumu na wadhifa huo hadi mwaka 1995.
 

Wakati wa uongozi wake akiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi alikuwa na busara, hekima na ujasiri katika kusimamia maamuzi ya chombo hicho muhimu cha kutunga Sheria.
 
Miongoni mwa baadhi ya mambo aliyoyasimamia katika kazi yake hiyo ni pamoja na kuliingiza Baraza hilo katika Mabaraza ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CPA) ambapo pia chini ya uongozi wake alifanikiwa kuendesha kikao ambacho kilichopitisha Sheria namba 15 ya mwaka 1992 iliyohusiana na mfumo wa siasa ya vyama vingi nchini Tanzania jambo ambalo limetengeneza historia kubwa hapa nchini.

 
Marehemu Ali Khamis hadi kufa kwake amejaaliwa kupata watoto 13 na wajukuu 39 na ameacha kizuka mmoja.
 
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Baraza la Wawakilishi ilitoa mkono wa pole kwa wafiwa wote na kuwataka wawe na subra katika msiba huo.

 

Nao wanafamilia walitoa shukurani kwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na viongozi wote na wananchi pamoja na Jeshi la Polisi kwa kutoa ushirikiano wao mkubwa katika mazishi ya mzee wao huyo.

 

 

Rajab Mkasaba

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>