Wajumbe wa Mkutano uliojadili zoezi la kuhamisha Makontena kutoka Eneo la Bandari ya Malindi na kuwekwa katika Viwanja vya Malindi mbele ya Majengo ya Manispaa ya Mji wa Zanzibar wakisikiliza viongozi walioitisha mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Kikwajuni. Picha na Miza Othman-Maelezo Zanzibar
Waziri wa Habari,Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbarouk akizungumza na washiriki wa mkutano uliojadili suala la kuwekwa Makontena katika Viwanja vya Malindi, kushoto ni Waziri wa Miundo Mbinu na Mawasiliano Zanzibar Juma Duni Haji. Picha na Miza Othaman-Maelezo Zanzibar.
Na Fatma Mzee-Maelezo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuyahamisha Makotena yaliyopo katika eneo la Viwanja vya Bwawani Hotel na kuyaweka katika Uwanja wa Malindi uliopo mbele ya Jengo la Manispaa mjini Zanzibar.
Maamuzi hayo yamefanywa baada ya makubaliano ya Waziri wa Habari Utalii, Utamaduni na Michezo, Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Mbunge na Mkurugenzi wa Mji mkongwe pamoja na Viongozi wa Michezo Zanzibar.
Waziri wa Habari,Utalii ,Utamaduni na Michezo Said Ali Mbarouk ameeleza kuwa sababu ya kuhamishwa Makontena hayo ni kuonekana kuwa kikwazo kwa Wawekezaji.
Amesisitiza kuwa Makontena hayo yatawekwa kwa muda tu ambapo Serikali inaendelea kutafuta eneo maalum la kuyaweka.
Nae Mbunge wa Mji Mkongwe Ibrahim Sanya ameiomba Serikali ingalie kwa kina suala hilo hasa ikizingatiwa kuwa kiwanja hicho kinatumiwa na Wananchi kwa shughuli mbali mbali ikiwemo Mikutano ya Hadhara na Michezo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mji Mkongwe Issa Sarboko Makarani alihimiza umuhimu wa kutunza haiba ya mji Mkongwe kwani ni kivutio kikubwa cha Watalii.
Waziri wa habari amewaomba wajumbe waliohudhuria katika mkutano huo kutoa mashirikiano pale yanapohitajika ili kuendelea kuuweka mji wa Zanzibar katika haiba nzuri