Na Mwanajuma Mmanga
Waislamu wanaokwenda Makka kutekeleza ibada ya Hijja,wametakiwa kutofanya udanganyifu wakati wanapofanya chanjo za maradhi mabali hasa katika kipindi hichi ambacho mataifa ya Afrika Magharibi yanapokabiliwa na ugonjwa hatari wa Ebola.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa Shughuli za Kiislamu, Kamisheni ya Wakfu Mali ya Amana Zanzibar, Khalid Mohammed Mrisho, alisema kutokana na kushamiri kwa maradhi hayo yanayoambukizwa ni vyema Mahujaji wakawa waaminifu wanapofanya chanjo.
Alisema kuna uwezekano mkubwa kwa mahujaji ambao wapepitia nchi zilizoathirika na Ebola kabla ya kuingia Saudi Arababi wakawekwa chini ya uangalizi maalum, hivyo kuondoa usumbufu chanjo ni muhimu.
Kuhusu viza, alisema kuchelewa kwa viza zao kunatokana na sababu za kiufundi zilizopo katika ubalozi wa Saudi Arabia, lakini juhudi zinaendelea kuchukuliwa.
Alisema baada ya kufanya mazungumzo na ofisi ya ubalozi, wameahidiwa kwamba mtandao huo utakaa sawa baada ya siku mbili.
“Hadi sasa hakuna Hujaji aliyepata viza kwa sababu ya kutokea hitilafu za kiufundi,” alisema.
Kundi la mwanzo la mahujaji litaondoka Septemba 16 kupitia taasisi ya Ahlu Dawa ambao watasafiri kwa ndege ya shirika la Oman Air.
Kundi la pili litawahusosha mahujaji wanaosafirishwa na jumuiya za Tawhid, Istiqama, Mother Care, Zanzibar Hajj na Labaika, ambao wataondoka na ndege ya Yemen Air Septemba 19.
Alisema na kundi la mwisho linasafirishwa na Jumuiya ya Al-haramain Septemba 24 mwaka huu kwa ndege ya Shirika la Ndege ya la Yemen Air.