Na Mwandishi Wetu. Dodoma
MWENYEKITI wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), John Cheyo, amesema mchakato wa katiba unaendelea vizuri na kwamba wakati walipozungumza na Rais Kikwete, walikubaliana uendelee hadi likamilishe kazi ya kutunga katiba inayopendekezwa.
Akichangia kwenye bunge la katiba jana, alisema ana imani kazi hiyo itakamilika katika kipindi hicho.
Akionekana kuwagusa moja kwa moja UKAWA, Cheo alisema bunge hilo haliendeshwi kwa kelele za barabarani bali linaendeshwa kwa sheria.
Alitaja sheria hiyo kuwa ni tangazo la Rais katika gazeti rasmi la serikali (GN 254) ambayo inataja uhai wa bunge kuwa unaishia Oktoba 4, 2014. Alimpongeza Rais Kikwete kwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuleta suluhu ya jambo hilo.
Aidha alisema kila moja alirekodiwa wakati wakizungumza katika majadiliano hayo, hivyo ameomba zitengenezwe CD na kusambazwa ili Watanzania wajue viongozi wao walivyozungumza.
Aliwashangaa UKAWA kwa kupiga kelele barabarani ilhali wakati wakizungumza na Rais Kikwete hawakuzungumza wanayoyazungumza mtaani.
Alisema waliyoyazungumza kwa waandishi wa habari ndiyo waliyokubaliana wakati wa mazungumzo na Rais Kikwete.
Alisema bunge la katiba lina watu makini na aliwataka kujiamini ili wakamilishe kazi zao kwa wakati.
Alisema kuna mambo mengi mazuri yamezungumzwa kwenye bunge maalum hasa yanayowahusu wakulima, wafugaji na wavuvi.
Pia alisema suala la muungano limepatiwa ufumbuzi ambapo Rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu atakuwa Makamu wa Pili wa Muungano.