Na Kauthar Abdalla
Hatimae wafanyakazi wa shamba la mipira la Kichwele wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja, wameanza kulipwa mishahara yao baada ya kufanya kazi kwa muda wa zaidi ya miezi sita.
Wafanyakazi hao wamelipwa mishahara ya miezi miwili kuanzia jana.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi hao wamegoma kuchukua mishahara hiyo na kusema wataendelea na mgomo.
Wafanyakazi hao walikuwa wamegoma kwa muda wa takribani mwezi mmoja, wakidai malimbikizo ya mishahara yao.
Mwandishi wa habari hizi, aliwashuhudia wafanyakazi hao wakilipwa, ambapo malipo yalifanywa kwa mujibi wa siku ambazo mfanyakazi alizalisha.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,Katibu wa wafanyakazi wa kampuni hiyo, Halima Hussein Kuchilewa,alisema licha ya kuwa kampuni inazalisha kama kawaida lakini wafanyakazi walikuwa hawalipwi mishahara yao kama kawaida.
Alisema kitendo kilichofanywa na mwekezaji cha kutolipa mishahara, kimesababisha hali ngumu za maisha pamoja na kushindwa kutunza familia zao.
Ofisa kutoka Kamisheni ya Kazi Mkoa Kaskazini Unguja, Ame Haji Ali, alisema ni kweli Kamisheni imepokea malalamiko ya wafanyakazi hao na imechukua juhudi za kuzungumza na uongozi wa kampuni na ndipo walipokubali kuwalipa miezi miwili ya kwanza.
Alisema licha ya baadhi ya wafanyakazi kumaliza mikataba, hakuna sababu ya kutolipwa mishahara yao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni hiyo, Sudi Mohammed Magumra, alisema tayari ufumbuzi wa tatizo hilo umeshapatikana na fedha zilizosalia zitalipwa katika kipindi cha mwezi mmoja ujao na kuwaomba wafanyakazi kurejea kazini.
Alisema sababu kubwa iliyofanya mishahara kuchelewa ni upungufu wa uzalishaji na soko la mpira katika viwanda vinavyonunua.