Na Fatina Mathias, Dodoma
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, amesema rasimu ya mwisho itakamilika Septemba 21 mwaka huu ambapo wajumbe wa bunge hilo watakuwa wamefikia lengo walilowekewa na taifa la kutoa katiba.
Akizungumza katika bunge hilo, Sitta alisema katika kikao cha jana (juzi) cha Kamati ya Uongozi, wamedhihirisha kwamba wanakwenda vizuri na Kamati ya Uandishi ambayo imekuwa ikitazama mambo yanavyokwenda, imejipanga kutoa rasimu ya mwisho Septemba 21.
“Ratiba yetu ya bunge maalumu inaendelea kama ilivyopangwa,siku 60 za bunge hili ambazo ni nyongeza ya siku tulizopewa kwa mujibu wa sheria zinaishia Oktoba 4,”alisema.
Aidha alisema akidi inahusu wajumbe wote ambao waliteuliwa na Rais kuwa wajumbe wa bunge hilo.
Alisema sekretarieti imeandaa muhtsari wa maoni yalivyotoka ndani ya kamati 12, kwa maana hivyo mwenendo wa ndani ya bunge maalum hautaibua mjadala mpya.
Aidha alisema baadhi ya wajumbe katika kamati zao wamerejea tena kuidai Mahakama ya Kadhi ndani ya katiba na wengine wanasema ndivyo ilivyo Uganda wakati sio kweli.
Aliwaomba wajumbe kutorudia tena yale yaliyojadiliwa kwenye kamati na kwamba hoja ikashindikana iwekwe pembeni.