Na Mahmoud Ahmad, Arusha
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, imemteua Jaji Mkuu (mstaafu) wa Tanzania, Agustino Ramadhan, kuwa Rais wa mahakama hiyo, kwa kipindi cha miaka miwili.
Anachukua nafasi ya Sophia Akuffo wa Ghana, aliemaliza muda wake.
Jaji Ramadhan anakuwa Mtanzania wa kwanza kushikilia kiti hicho tokea kuanzishwa mahakama hiyo baada ya kupata kura saba dhidi ya kura nne alizopata mpinzani wake.
Makamu wake anakuwa Jaji Eisie Thompson, kutoka Nigeria.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya uteuzi huo, Jaji Ramadhan, alisema ni heshima kwa Tanzania kwani ndio mara yake ya kwanza kupata nafasi hiyo.
“Kesi yeyote inayohusu nchi yangu mimi sitakuwepo kutokana na sheria zetu za mahakama hii. Tayari Watanzania watano wamefungua kesi katika mahakama hii na mbili zimetolewa hukumu ikiwemo ya Mchungaji Mtikila na Zongo,”alisema.
Aidha mahakama hiyo iliwaapisha Majaji watatu kabla ya kuanza mchakato wa upigaji kura kumteuwa Rais wa mahakama hiyo.