Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Bandari yataka uwanja wa Malindi kuhifadhia makontena

$
0
0
Na Mwashamba Juma
Mjadala umeibuka kufuatia Shirika la Bandari Zanzibar kutaka lipatiwe uwanja wa Malindi kwa ajili ya kuhifadhia makontena.

Mjadala huo uliibuka wakati Shirika hilo lilipokutana na wadau wa uwanja huo katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Kikwajuni.

Akizungumza katika mjadala huo, Waziri wa Habari, Utalii, Mhe. Said Ali Mbarouk, alisema uchumi wa serikali unategemea kwa kiasi kikubwa sekta za utalii, bandari na viwanja vya ndege.

Hivyo, alisema serikali imeamua makontena hayo yahifadhiwe katika uwanja huo kwa sababu eneo linalotumika sasa ambalo lipo mbele ya hoteli ya Bwawani, amepewa mwekezaji ambae atajenga hoteli ya daraja la juu ili kuvutia wageni wengi zaidi.

Aidha alisema serikali inaendelea na mazungumzo na mwekezaji kuhusu ujenzi wa hoteli hiyo.

Akitoa sababu za kiuchumi, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Salmini Senga Salmini, alisema ongezeko la makontena lililosababishwa na kukua kwa uchumi duniani, limesababisha ongezeko la mizigo bandarini.


Aidha, alisema kwa kuwa bandari hiyo inaendelea kujengwa, kumesababisha ufinyu wa nafasi wa kuhifadhia makontena.

Alisema hatua mbadala zilizochukuliwa na Shirika ni kupendekeza maeneo ya Saateni na Kisauni lakini ilishindikana kutokana na usumbufu wa usafiri na gharama za uendeshaji.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Abdalla Juma Abdalla, alisema kuna hatari ya shirika kupoteza meli kubwa za mizigo kama halitokuwa na eneo mbadala ya kuhifadhi makontena.

“Kwa sasa tunapokea makontena 3,000 kwa mwezi hatujui mwezi ujao kama yatakua 2,000 au 1,000, awali tulikuwa tunapokea makontena 8,000 na kushuka hadi 5,000, sasa bora tuendee kuhifadhi viwanja kwa ajili ya michezo ya watoto wetu au tusubiri hadi shirika lishindwe kulipa mishahara wafanyakazi wake kisha wagome, halafu tununue mchele kwa kilo 3,000,” alihoji.

Mkurugenzi Mamlaka ya Mji Mkongwe, Issa Sarboko, alisema hali inavyoelekea huenda hadhi ya mji Mkongwe ikapotea.

“Napata wakati mgumu kutokana na misukumo kutoka UNESCO na taasisi za serikali juu  ya hifadhi ya mji Mkongwe,” alisema.

Mbunge wa mji Mkongwe, Mhe. Ibrahim Sanya, alipinga uamuzi wa serikali kuweka makontena eneo hilo kutokana na sababu za kiusalama.

“Serikali irudi na kuzungumza na mwekezaji wake juu ya ujenzi mpya wa hoteli ya Bwawani, ikiwezekana imwambie kuwa ianze na jengo kabla kuendelea na hatua nyengine wakati na sisi tunaendelea na mazungumzo na UNESCO,” alishauri.

Wadau wa michezo kutoka shehia za Malindi na Mchangani, walisema uwanja huo ndio pekee unaohudumia shehia nne za mji Mkongwe na kuongeza kuwa wazee na kamati za shehia hizo hawajaridhishwa na uamuzi huo.


Kwa upande wake Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Mhe. Juma Duni, alisema kupungua kwa meli za kigeni kunasababishwa na msongamano uliopo bandarini, hali inayosababisha makontena kushushwa Dar es Salaam na Mombasa.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>