STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 15 Septemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewasili visiwa vya Comoro leo mchana kuanza ziara ya kikazi ya siku nne kufuatia mwaliko wa Rais wa Muungano wa Comoro Mheshimiwa Ikililou Dhoinine.
Katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Prince Said Ibrahim mjini Moroni, Dk. Shein alipokelewa na mamia ya wananchi wa mji wa Moroni na viongozi wa Serikali wakiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano wa Comoro Mheshimiwa Mohamed Ali Soilihi pamoja na Balozi wa Tanzania nchini humo Mheshimiwa Balozi Chabaka Kilumanga.
Mara baada ya kuwasili Dk. Shein alikaribishwa kwa kupigiwa wimbo wa Taifa na kuvishwa shada la maua kulingana na utamaduni wa watu wa Comoro baadae kusalimiana na viongozi wa Serikali na kidini waliofika kumlaki.
Katika mazungumzo mafupi kiwanjani hapo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano wa Comoro,viongozi hao wawili walieleza haja ya kuimarisha ushirikiano wa kindugu na wa damu uliopo kati ya Visiwa vya Comoro na Zanzibar.
Dk.Shein alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Muungano wa Comoro kuwa ziara yake hiyo ya siku nne itasaidia kuimarisha uhusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufungua milango zaidi ya ushirikiano kati ya nchi hiyo na Zanzibar.
Kabla ya kuondoka kwenda mjini Moroni, Dk. Shein alikagua vikundi mbalimbali vya sanaa na utamaduni na kusalimiana na wananchi wengine walioshiriki mapokezi yake.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa hapa, baadae leo jioni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi atakutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Muungano wa Comoro Mheshimiwa Ikililou Dhoinine.
Mazungumzo hayo na Rais Dhoinine yanatarajiwa kuwa juu ya kukuza uhusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Muungano wa Comoro na pia kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na nchi hiyo.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Rais amefuatana na mke wake Mama Mwanamwema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, Naibu wa Waziri wa Kilimo na Maliasili Bibi Mtumwa Kheir Mbarak na Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwezeshaji na Uchumi Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.
Wengine ni Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Bwana Ali Saleh Mwinyikai, Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Asha Ali Abdulla na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Zanzibar Bwana Kombo Abdulhamid Khamis.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822