Na Said Ameir, Comoro
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, yuko Comoro kuanza ziara ya kikazi ya siku nne kufuatia mwaliko wa Rais wa visiwa hivyo, Mhe. Ikililou Dhoinine.
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Prince Said Ibrahim mjini Moroni, Dk. Shein alipokelewa na mamia ya wananchi wa mji wa Moroni na viongozi wa serikali wakiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Comoro, Mhe.Mohamed Ali Soilihi pamoja na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Chabaka Kilumanga.
Mara baada ya kuwasili alikaribishwa kwa kupigiwa wimbo wa taifa na kuvishwa shada la maua kulingana na utamaduni wa watu wa Comoro baadae kusalimiana na viongozi wa serikali na kidini waliofika kumlaki.
Katika mazungumzo mafupi uwanjani hapo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Comoro,viongozi hao wawili walieleza haja ya kuimarisha ushirikiano wa kindugu na wa damu uliopo kati ya Comoro na Zanzibar.
Alimueleza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Comoro kuwa ziara yake itasaidia kuimarisha uhusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufungua milango zaidi ya ushirikiano kati ya nchi hiyo na Zanzibar.
Kabla ya kuondoka kwenda Moroni, Dk. Shein alikagua vikundi vya sanaa na utamaduni na kusalimiana na wananchi wengine walioshiriki mapokezi yake.
Jana jioni atakutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Comoro, Ikililou Dhoinine.
Mazungumzo hayo yalikuwa juu ya kukuza uhusiano kati ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Comoro na pia kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na nchi hiyo.
Katika ziara hiyo, Dk. Shein amefuatana na mke wake, mama Mwanamwema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora, Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, Naibu wa Waziri wa Kilimo na Maliasili, Mhe. Mtumwa Kheir Mbarak na Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwezeshaji na Uchumi, Mhe.
Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.
Wengine ni Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khamis Haji, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Ali Saleh Mwinyikai, Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto, Asha Ali Abdulla na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Zanzibar,Kombo Abdulhamid Khamis.