Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar Chen Qi Man, nyumbani kwake Mbweni. Balozi Chen alikutana na Maalim Seif kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi nchini.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akimkabidhi zawadi Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar Chen Qi Man, nyumbani kwake Mbweni. Balozi Chen alikutana na Maalim Seif kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej akipokea zawadi kutoka kwa Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar Chen Qi Man, wakati wakiaagana kufuatia balozi huyo kumaliza muda wake wa utumishi nchini.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiagana na Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar Chen Qi Man, nyumbani kwake Mbweni, kufuatia balozi huyo kumaliza muda wake wa utumishi nchini. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej na kushoto ni Afisa ubalozi wa China aliyepo Zanzibar. Picha na Salmin Said, OMKR
Na Hassan Hamad OMKR
Maalim Seif amekutana na Balozi mdogo wa China aliyepo Zanzibar Chen QiMan na kuelezea umakini na uadilifu wa makampuni ya Kichina katika kutekeleza majukumu yao.
Amesema mara nyingi kazi za kiufundi wanazopewa wataalamu wa Kichina zimekuwa zikitekelezwa kwa umakini na kwa wakati uliopangwa, hali inayotoa matumaini ya kuendelea kutoa tenda kwa makampuni hayo.
Aidha amesifu ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya China na Zanzibar ambao umekua ukichangia maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.
Amemtaka balozi huyo kuwa kiungo katika kuwashajiisha watalii na wawekezaji wa China kuja Zanzibar, ili kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema China ni mshirika wa kweli wa maendeleo ambayo imekuwa ikishirikiana na Zanzibar katika kutatua kero zinazoikabili ikiwa ni pamoja na kusaidia wataalamu hasa katika sekta ya afya.
Naye balozi QiMan amesema katika kipindi chake cha utumishi hapa nchini, ameshuhudia mafanikio makubwa yakipatikana yakiwemo kuimarika kwa majengo, huduma za elimu pamoja na miundombinu ya mawasiliano.
Ameahidi kuwa China itaendelea kushirikiana na Zanzibar na kutoa michango zaidi katika kusaidia uimarishaji wa uchumi wa Zanzibar.
Balozi Chen QiMan amemaliza muda wa utumishi hapa nchini, baada ya kuitumikia nafasi hiyo ya ubalozi mdogo kwa kipindi cha miaka miwili na nusu.