Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Matukio ya kumwagiwa Tindikali, Maalim Seif ataka uchunguzi wa kina ufanyike

$
0
0
Na Hassan Hamad, OMKR
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema anasikitishwa na matukio ya hujuma yaliyojitokeza Zanzibar, ikiwemo watu kumwagiwa tindikali, na kutaka uchunguzi wa kina ufanywe kuwabaini wahusika, na baadaye ripoti ya uchunguzi huo iwekwe wazi kwa wananchi.
 
Amesema hatua ya kuwekwa bayana ripoti za uchunguzi wa matukio hayo ya hujuma, ni jambo muafaka katika kufuta dhana zinazojengeka miongoni mwa wananchi na jamii ya kimataifa kuhusiana na watu wanaohusika kufanya hujuma hizo.
 
Maalim Seif ameyasema hayo katika mahojiano maalum juu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu kuasisiwa kwake mwaka 1964.
 
Amesema ili amani na mshikamano wa wazanzibari udumu, matukio kama hayo ya hujuma ambayo yamekuwa yakiwalenga zaidi baadhi ya viongozi wa dini na hata wageni, hayanabudi kuangaliwa kwa upana wake, na kuwataka wananchi wajiepushe na kufikia maamuzi ya haraka kuwahusisha wengine bila ya uchunguzi wa kina kufanywa.
Alisema wananchi walipata matumaini ya kukomeshwa kwa vitendo hivyo mara baada ya hujuma zilizofanywa dhidi ya viongozi wa dini pamoja na mripuko uliotokea katika kanisa la Arusha ambapo walihidiwa uchunguzi wa kina utafanyika na kuhusisha wapelelezi wa kimataifa, lakini hadi sasa hakuna ripoti yoyote iliyowekwa bayana.
 
Maalim Seif ameeleza kwamba badala yake matukio ya hujuma yameendelea na wananchi kuendelea kujenga dhana ya kuwahusisha watu au makundi maalum bila ya kuwa na uthibisho, jambo ambalo ni hatari kwa usalama na utulivu wa nchi.
 
“Ingekuwa wakati ule tungesema ni siasa, lakini sasa tuna serikali ya pamoja Zanzibar, kwa nini mambo haya yanatokea sasa, huu ni mtihani mkubwa kwetu”, alisema Maalim Seif.
 
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF, amesema pia amekuwa mgumu kuamini kuwa dini inahusika katika matukio ya hujuma yaliyotokea Zanzibar.
 
Amesema Zanzibar ina historia ya kipekee ya uvumilivu wa kidini duniani, kutokana na wananchi wa visiwa hivi kuishi pamoja kwa miaka mingi bila ya kubaguana kwa misingi ya dini zao.
 
“Sisi Zanzibar kiwango chetu cha uvumilivu ni kikubwa na nambari moja duniani, hata ukiangalia Ukristo Afrika Mashariki mlango wake ni Zanzibar”, alifafanua Maalim Seif.
 
Akitoa mfano wa uvumilivu huo, Maalim Seif amesema hata unafika mwezi wa Ramadhan huwezi kumuona mtu wa imani yoyote akila hadharani wakati wa mchana, na kwamba wananchi wote wanashirikiana katika shughuli za kijamii bila ya kujali imani zao.
 
Ameeleza kuwa baada ya matukio ya kujeruhiwa Padri Ambrose Mkenda, kuuawa kwa Padri Evarist Mushina mripuko wa bomu katika kanisa mjini Arusha, Serikali iliahidi kuleta makachero wa F.B.I, na hata baada ya wasichana wa Kiingereza kumwagiwa tindikali inaelezwa wachunguzi kutoka Scktland Yard wapo, lakini hakuna taarifa hadi sasa iliyotolewa kuhusiana na uchunguzi huo.
 
“Tusiajiegemeze kwenye dhana, uchunguzi ndio kitu muhimu. Hawa wanaoathirika na hujuma mbali ya kuwa viongozi wa dini nao ni binadamu, tujiulize jee hawakujenga uhasama au kutokufahamiana na wengine huko katika jamii”, alihoji Maalim Seif.
 
Amefahamisha kuwa ni makosa kuendesha mambo kwa dhana, kwa vile matokeo yake ni kuwaadhibu watu kwa kuwaweka ndani bila ya kuwa na hatia.
 
Amewataka wananchi kuwa makini na waendelee kuwa wamoja, ili amani, mashirikiano na umoja uliodumu uendelee wakati huu ambapo Zanzibar inaadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>