Na Rajab Mkasaba, Ikulu
UONGOZI wa Benki wa Taifa ya Biashara (NBC) umeeleza kuvutiwa kwake na hatua za maendeleo ya kiuchumi zilizofikiwa Zanzibar na kuahidi kuendelea kuziunga mkono ili ziweze kuimarika zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Mizinga Melu, aliyasema hayo wakati alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiwa pamoja na uongozi wa benki hiyo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, alimueleza Dk. Shein kuwa NBC inathamini juhudi na mafanikio yaliofikiwa na kusisitiza kuwa benki yao ina kila sababu ya kuendelea kutoa ushirikiano wake kwa serikali pamoja na wananchi wa Zanzibar.
Alisema NBC imepata mafanikio makubwa Zanzibar hali ambayo imetokana na ushirikiano uliopo ambao umeisaidia benki hiyo kupiga hatua kubwa na kuimarika zaidi.
Aliahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha huduma za maendeleo.
Nae Dk. Shein aliueleza uongozi wa benki hiyo, kuwa juhudi za benki hiyo na mafanikio yaliopatikana ipo haja ya kuyaimarisha zaidi kutokana na ushindani mkubwa wa kibiashara uliopo.
Aliueleza uongozi huo kuwa licha ya ushindani huo NBC imeweza kupiga hatua katika kujiimarisha.
Alitoa wito kwa uongozi huo wa NBC kuendelea kutoa huduma zaidi kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano na kujitangaza katika maeneo ya vijijini.
Aliuahidi uongozi huo kuwa serikali itaendeleza ushirikiano na benki hiyo pamoja na benki nyengine zote ambazo zinafanya shughuli zake Zanzibar kwa lengo kukuza uchumi na kuimarisha maendeleo.