Na Mwashungi. Twahir
Kamisheni ya Utalii Zanzibar inatarajia kuadhimisha siku ya Utalii duniani kuanzia tarehe 26 na kufikia kilele chake tarehe 28 katika kijiji cha Nungwi wilaya ya Kaskazini Unguja.
Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Dkt. Ahmada Hamad Khatib wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Amani .
Amesema sherehe hizo ambazo kimataifa zinafanyika nchini Mexico, zitaanza kwa maonesho ya biashara kutoka kwa wajasiria mali itakuwa kivutio kikubwa kwa wageni watakaokuwepo Zanzibar.
Ameongeza kuwa sherehe hizo zitaambatana na semina, usafi wa mazingira, ngoma za utamaduni na michezo ikiwemo mpira wa ufukweni, mashindano ya kuogelea, mashindano ya ngalawa, sarakasi na mchezo wa kuvuta kamba.
Amefahamisha kuwa katika maadhimisho hayo kamati ya usafi ya kijiji cha Nungwi itakabidhiwa vifaa vya usafi pamoja na kutolewa zawadi kwa washindi na Taasisi zlizochangia katika sherehe hizo.
Sambamba na hayo alisema Serikali pamoja na taasisi binafsi zimefanya juhudi kubwa katika suala zima la kuimarisha usafi wa mazingira na kuhakikisha Mji wa Zanzibar unakua safi na kuwa kivutio kwa wageni.
Dkt. Ahmada alisema kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni Utalii na maendeleo ya nchi, ikitanabahisha shughuli zote zinazofanyika za utalii ziwe zinawanufaisha wananchi wenyewe.ambapo sherehe hizo zinaadhimiswa nchini mexico.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Nd.Saleh Ramadhan Feruzi alisema kasi ya ukuaji Utalii nchini imeongezeka kutoka 169,000 mwaka 2012 na kufikia 181,000 mwaka 2013 na inategemewa kuongezeka zaidi mwaka huu 2014.
‘’Tumejiandaa katika kuimarisha ulinzi wa watalii kwa kupeleka mswaada wa sheria katika Baraza la Wakilishi ili watalii wanaokuja Zanzibar wawe katika hali ya usalama zaidi na mali zao,”alisema Feruzi.
Ameongeza kuwa kuimarika kwa ulinzi wa watalii kutasaidi katika ulinzi kwa wawekezaji wa sekta ya utalii.