STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 29 Septemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Zanzibar inakaribisha miradi mikubwa katika sekta ya utalii sio tu kwa sababu inabadili sura ya uwekezaji katika sekta hiyo lakini miradi hiyo inakwenda sambamba na utekelezaji wa malengo ya Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020.
Akizungumza na ujumbe wa Kampuni ya Penny Royal kutoka uingereza ofisini kwake Ikulu leo, Dk. Shein ameipongeza kampuni hiyo kwa kuamua kuwekeza mradi mkubwa wa aina yake wa utalii utakaokuwa na huduma za kisasa ambazo hivi sasa hazijakuwepo katika sekta hiyo hapa Zanzibar.
Mardi huo utakaojulikana kama Amber Golf and Beach Resort utajengwa huko Matemwe Muyuni na utajumuisha hoteli, kiwanja kidogo cha ndege, nyumba za kununua zilizo baharini, sehemu ya kuegesha boti za kifahari, uwanja wa kuchezea gofu pamoja na sehemu za kutolea huduma mbalimbali zikiwemo sehemu za kuuzia bidhaa za asili kwa ajili ya watalii.
Dk. Shein aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano kadri watakavyohitaji na kuongeza kuwa wananchi wa Zanzibar kama walivyo watu wa visiwa duniani ni watu wanaopenda kuishi na wageni hivyo kuwahakikishia ushirikiano kutoka kwao.
Aliuambia ujumbe wa kampuni hiyo ulioongozwa na mmiliki wa mradi huo bwana Brian Malcon Thomson kuwa Zanzibar inaukaribisha mradi huo kwa mikono miwili kwa kuamini kuwa kufanikiwa kwake kutaongeza vivutio vya utalii nchini na kuimarisha sekta hiyo kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar.
Alisema ametiwa moyo na azma ya wamiliki wa mradi huo wa kuwatumia vijana wa Zanzibar tangu mwanzo wa ujenzi kwa nia ya kuwapatia ujuzi na utaalamu katika kujenga miradi kama hiyo pamoja na kusaidia miradi ya vijana ikiwemo kilimo.
Aliongeza kuwa wazo la kuwapatia wananchi hasa kinamama sehemu za kufanyia shughuli zao katika maeneo ya mradi ni la kuungwa mkono kwa kuwa linatekeleza mpango wa serikali wa utalii kwa wote unaohimiza ushirikishwaji kikamilifu wa wananchi katika sekta nzima ya utalii.
Dk. Shein alisema kuwa amefurahi kuona mchezo wa gofu unarejea tena Zanzibar kupitia mradi huo na kufafanua kuwa mchezo huo ulikuwa maarufu Zanzibar na uliweza kuvutia wachezaji mashuhuri kutoka nchi za Afrika Mashariki na kwengineko.
Kwa upande wake, Bwana Brian Thomson alimueleza Mheshimiwa Rais kuwa ameridhishwa na ushirikiano alioupata hadi sasa kutoka kwa viongozi na wananchi na kueleza kuwa matayarisho ya mradi huo yako katika hatua za juu.
Katika ujenzi wa mradi huo, alisema wanataka kuingiza tekinolojia ya kisasa na wangependa kuona vijana wa Zanzibar wanashiriki kikamilifu ili waweze kujifunza tekinolojia hiyo kwa manufaa yao binasfsi na Zanzibar kwa ujumla.
Kuhusu kuwaendeleza wananchi wa karibu na mradi huo hasa wanawake, alisema wametenga sehemu maalum kwa ajili ya shughuli za kinamama katika eneo la mradi na kuahidi kuwasaidia kuendeleza vipaji vyao pamoja na kusaidia vijana shughuli za kilimo.
Bwana Thomson ambaye alikuwa amefuatana na Mkandarasi wa Mradi huo Bwana David Haycock, alibainisha kuwa tayari wameshafanya mawasiliano na wananchi hao kwa kushirikiano na viongozi wa maeneo yao na kuona baadhi ya bidhaa wanazozalisha hivyo suala hilo limezingatiwa katika mradi mzima.
Alieleza kuwa lengo la kujenga uwanja wa kisasa na kimataifa wa gofu ni kuvutia wacheza gofu mashuhuri ulimwenguni ambapo hilo likifanikiwa itakuwa ikiitangaza Zanzibar ulimwenguni kote kutokana na mchezo huo ulivyokuwa mashuhuri.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Bwana Ali Khalil Mirza.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822