Na Othman Khamis, OMPR
MJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba, Hamad Rashid Mohamed, amesema dhambi kubwa itafanywa na wajumbe wa bunge hilo kama watawakosesha Watanzania rasimu ya katiba mpya wanayoisubiri kwa shauku kubwa.
Alitoa kauli hiyo wakati akitoa nasaha zake kwa niaba ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wa kundi la 201 kutoka Zanzibar, kwenye chakula cha jioni kilichoandaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, nyumbani kwake mtaa wa Farahani mjini Dodoma.
Alisema wajumbe hao wamebeba dhima kubwa kwa kukubali kwao kula kiapo kilichokwenda sambamba na kutumia kodi za wananchi zilizotolewa kwa kutakiwa kuwatengenezea katiba mpya.
Alisema wajumbe wa bunge hilo hasa wale waliotoka vyama vya upinzani na taasisi za kijamii wanapaswa kusimamia vyema ukamilishaji wa rasimu inayopendekezwa na bunge ili kukata kiu waliyonayo Watanzania kwa kipindi kirefu sasa.
Alisema vyama vya upinzani zikiwemo taasisi za kijamii na wana harakati ndio waliosimama kidete kudai uwepo wa katiba mpya jambo ambalo lilikuwa zito kukubaliwa na CCM.
“Hakuna nji nyengine yoyote ya mkato katika kukipa changamoto chama cha Mapinduzi isipokuwa upande wa upinzani kukubaliana na rasimu iliyoandaliwa na Bunge maalum la katiba itakayopelekwa kwa wananachi kwa ajili ya kupigiwa kura,” alisema.
Alitahadharisha kwamba Watanzania wamejinyima mambo ya msingi likiwemo kuwapatia elimu watoto wao na kuamua kodi wanazochangia kuzielekezwe kupata katiba mpya.
Aliwanasihi viongozi wa kisiasa pamoja na jamii kuzikimbia chokochoko za kisiasa zinazochangia cheche ya kusambaratisha jamii kama zilivyotokea mataifa mbali mbali Duniani.
Alisema Tanzania hadi sasa bado haijafikia hatua za watoto pamoja na wake wa Wabunge kuteswa, kudhalilishwa hadi kufikia hatua ya kubakwa kutokana na vurugu zinazotokana na siasa na hitilafu za kidini kama zinavyofanyika katika mataifa mengine.
Alisema Tanzania ina fursa kubwa ya kidemokrasia iliyojengeka tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ambayo imekuwa ikipatikana ndani ya vyombo vyake vya maamuzi.
Mapema akiwakaribisha wajumbe hao wa bunge hilo, Balozi Seif alisema rasimu iliyoandikwa na bunge hilo imeisaidia Zanzibar kwa zaidi ya asilimia 90 na kusababisha malalamiko kwa Watanzania Bara.
Alisema wakati huu ni muhimu na ndio mahali pekee pa kupata maslahi ya Zanzibar ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, vyenginevyo Zanzibar itaendelea kulalamikia kero za Muungano endapo rasimu inayopendekezwa na Bunge maalum haitapita.
Aliwakumbusha wajumbe wa bunge hilo kwamba Zanzibar ilikuwa na malalamiko mengi kuhusu kero za Muungano masuala ambayo sasa ni muda muwafaka wa kuyamaliza kupitia mchakato huo.
Alisema koti la Tanzania Bara linalodaiwa kuvaliwa ndani ya mambo yasiyo ya Muungano litavuliwa iwapo rasimu hiyo itapigiwa kura na kupita.