Na Mwandishi wetu
TANZANIA iko tayari kushirikiana na wanachama wote wa Umoja wa Mataifa (UN) kufikia makubaliano ya Malengo ya Maendeleo mapya baada ya Malengo ya Milenia (MDGs) ya sasa kufikia mwisho wake ifikapo mwaka 2015.
Rais Kikwete alisema hayo wakati akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York, Marekani.
Agenda ya kikao cha Baraza Kuu la UN mwaka huu ni "Delivering on and Implementing a Transformative Post 2015 Development Agenda" ambapo alisema anatarajia majadiliano yatatoa nafasi kwa nchi kupanga mipango ya baadae kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
"Tutumie muda huu kuendeleza mafanikio na mafunzo kutoka nchi mbalimbali na pia tujifunze kutokana na changamoto za kushindwa kufikia malengo ya milenia, na kuzitumia kama viashiria vya ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015," alisema.
Aliiasa dunia kuwa wakati huu ambapo inajadili ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, isisahau malengo ya milenia ambayo hayajakamilika na kuyaweka vizuri katika ajenda mpya ya baada ya malengo ya sasa kufikia tamati mwaka ujao.
Pamoja na kwamba dunia inazungumzia ajenda mpya ya baada ya mwaka ujayo, alizitaka nchi kuhakikisha na kuongeza kasi ya utekelezaji katika kipindi cha siku 461 zilizobakia kufikia mwisho.
Pamoja na umuhimu wa MDGs Rais Kikwete alizungumzia suala la tabianchi na kuzitaka nchi zote duniani kukusanya nguvu katika suala hilo ili kuiokoa dunia kutokana na majanga ya tabianchi.
Masuala mengine ni kuhusu mageuzi katika UN, ambapo alisema kusuasua kwa mazungumzo ya kuleta mageuzi kunakatisha tamaa na kuomba yafufuliwe.
Masuala mengine ni kuhusu hali ya usalama duniani ambapo ugaidi umechukua mkondo wa kutishia amani duniani na kuzitaka nchi zote kupambana na ugaidi.
Masuala mengine ni uhasama baina ya Israeli na Palestina ambalo limedumu kwa muda mrefu hivyo kuutaka Umoja wa Mataifa kulitafutia suluhu ya kudumu; suala la Sahara Magharibi ambalo pia limedumu kwa muda mrefu bila ufumbuzi na vikwazo kwa Cuba ambavyo navyo vimekuwepo kwa muda mrefu sana.
Alizungumzia ugonjwa wa Ebola ambao tayari umeua watu wapatao 2,400 na bado haujadhibitiwa.
Alisema ugonjwa wa Ebola ni tishio kwa nchi zilizoathirika, jirani na dunia kwa ujumla hivyo, juhudi za pamoja zinahitajika kwani ndio njia sahihi ya kuutokomeza.