Na Mariam Cyprian, Tanga
MTU mmoja asiyefahamika jina wala mahala anapoishi anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 35 amefariki dunia na mwili wake kusokomezwa kwenye kalavati la daraja na baadhi ya viungo vyake yaani kichwa na sehemu za siri vimeondolewa.
Tukio hilo limetokea wilayani Lushoto mkoani Tanga.
Akithibitisha Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Fresser Kashai, alisema tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji cha Katurupesa Kwemkwazu, majira ya saa 8:00 usiku ambapo uligundulika mwili wa mwanamme asiyefahamika jina wala mahali anapoishi akiwa ametupwa katika kalavati hilo.
Alisema chanzo cha tukio hilo bado hakijafahamika na jeshi la polisi kwa kushirikiana na wanachi wa eneo hilo wanaendelea na uchunguzi kubaini viungo vya mtu huyo vimepelekwa wapi.
Alisema mwili wa marehemu umezikwa na wananchi wa kijiji hicho baada ya kufanyiwa uchunguzi na madaktari wilayani humo, ambapo mpaka sasa watuhumiwa kuhusiana na tukio hilo bado hawajakamatwa.
Katika tukio jingine mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Amiri Bakari (65) mkazi wa kijiji cha Komkonga kata ya Mkata wilayani Handeni amefariki dunia baada ya pikipiki waliyokuwa wakiitumia wakati wakienda kuwinda wanyama pori kuanguka baada ya kushindwa kupanda mlima.
Akitoa taarifa ya hali ya uhalifu mkoa wa Tanga, Kamanda Kashai, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema lilitokea Septemba 27 mwaka huu majira ya saa 4:00 za asubuhi.
Alisema mtu huyo alikuwa na mwenzake katika pikipiki wakielekea porini kuwinda huku kila mmoja akiwa amebeba silaha yake aina ya gobole na ndipo walipofika kilima cha Lugala pikipiki yao ilishindwa kupanda mlima huo na kuanza kurudi nyuma na kuanguka.
Alisema katika tukio hilo silaha aliyokuwa ameibeba dereva wa pikipiki hiyo ayefahamika kwa jina la Kiduo Rajabu (35) ilifyatuka na kwa kuwa ilikuwa na baruti gololi ilimjeruhi abiria huyo ubavu wake wa kushoto na kusababisha kifo chake.
Alisema mtuhumiwa katika tukio hilo amekamatwa na upelelezi kuhusiana na tukio hilo.