Na Mwantanga Ame
BUNGE Maalum la Katiba jana lilianza kupigia kura rasimu inayopendekezwa kuanzia sura ya kwanza hadi ya 10, huku kura ya ndio ikiongoza ingawa baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar na Tanzania Bara walipiga kura ya hapana.
Idadi ya Wabunge wote wa Bunge Maalum ni 629, kati ya hao idadi ya wabunge wa Tanzania Bara ni 419 na Zanzibar ni 210.
Akidi inayotakiwa kupitisha rasimu ya katiba inayopendekezwa ni 280 kwa Tanzania Bara na 140 kwa Zanzibar.
Hali hiyo, ilijitokeza jana wakati wajumbe wa bunge hilo, walipoanza kuzipigia kura sura ya kwanza hadi ya 10 zenye ibara ibara 157.
Aidha wajumbe wengi hasa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipiga kura ya wazi huku wajumbe waliopiga kura ya siri wengi wao wanatoka kundi la 201.
Kabla ya kupiga kura hiyo, Wabunge wa Zanzibar walikaa upande mmoja huku wale kutoka Tanzania Bara nao wakikaa upande mwengine.
Mapema Waziri Mkuu, Mhe. Mizego Pinda, alifunga mjadala kuhusu mahakama ya kadhi, baada la kuliambia Bunge Maalum la Katiba, kwamba suala hilo litamalizwa kisheria katika kikao cha bunge mwezi Januari.
Alikuwa akitoa maelezo ya serikali kuhusu mahakama ya kadhi, baada ya wajumbe wengi wa bunge hilo, kulilia kuwepo mahakama hiyo ndani ya rasimu ya katiba inayopendekezwa, huku wengine wakitishia kutoipigia kura.
Alisema serikali kwa kuzingatia umuhimu wa kuwepo mahakama hiyo, imeona suala hilo linahitaji kuangaliwa kwa umakini ndani ya sheria mbili ambazo zinasimamia mambo ya kiislamu na serikali itahakikisha bunge la Januari inawasilisha mswada wa kuanzishwa taasisi hiyo.
Alisema hivi sasa shughuli za mahakamaya kadhi, zinafanyika katika maeneo mbali mbali ya Tanzania tangu mwaka 2012, lakini kilichojitokeza ni kuwepo ugumu wa baadhi ya maamuzi yalipofikishwa katika ngazi mbali mbali za kiutendaji.
Alisema yeye binafsi alikuwa mbumbu wa shughuli za mahakama ya kadhi, na ndio kwanza ameanza kutambua utendaji kazi wake.
Alisema hivi sasa Tanzania ina sheria mbili zinazosimamia mambo hayo, ikiwemo ya mahakama za mahakimu na sheria za kiislamu, ambazo zitafanyiwa marekebisho kwa kuziangalia upungufu wake na Bunge la Januari zitawasilishwa.
“Kwangu mimi ni faraja kubwa jambo hili lilianza kujitokeza tangu 2005 na kujitokeza katika vyombo vya sheria na kwenda nalo hadi 2010 na kuja 2012, na baada ya uchaguzi ndugu zetu walitaka kuanzishwa mahakama za kadhi, ambazo hivi sasa ziko sehemu mbali mbali, ila hoja ilikuwa maamuzi yaliokuwa yakitolewa hayakuwa yakifanyiwa kazi,”alisema.
Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa uamuzi wake wa kuanzisha mchakato wa katiba ndani ya kipindi cha miaka 50 ya Muungano na kuwapongeza wajumbe wa bunge hilo kwa kuimaliza kazi hiyo katika mazingira ya amani.
Tamko hilo, liliungwa mkono na viongozi wa dini waliokuwemo katika bunge hilo, akiwemo Sheikh Hamid Jongo, ambaye alisema wanakubaliana na uamuzi wa serikali kupitia tamko hilo kwa vile limeonesha dhamira ya kujenga umoja.
Nae Sheikh Mussa Kundecha, akitoa maelezo yake, alisema tamko la Waziri Mkuu ni zito na Waislamu wanapaswa walikubali.
Nae Askofu Mtetemela, alisema ni kweli suala la uwepo wa mahakama ya kadhi, liliwapa wasiwasi watu wa pande zote za dini, jambo ambalo lingeweza kuleta mpasuko wa kidini ambao ni mbaya kitaifa.
Mapema Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalum la Katiba, imekataa pendekezo la baadhi ya wabunge hilo lililokuwa likitaka kuruhusiwa kuwarejesha wanasiasa katika utumishi wao, baada ya kumaliza kutumikia nafasi hizo.
Kamati hiyo ilipinga hilo, wakati ikiwasilisha maoni ya mwisho baada ya kufanya masahihisho ya rasimu ya katiba yaliopendekezwa na wabunge wa bunge maalum, ambapo mjumbe Amon Mpanju, alisema hawakubaliana na pendekezo hilo, kwa vile wanaona linaweza kuwa kikwazo katika utekelezaji wake kwa kumfanya mtumishi kushindwa kuwajibika vyema.
Alisema Mbunge atakaemaliza utumishi wake katika ngazi ya kisiasa atakuwa bado ana imani ya chama alichogombea na atakaporudi kazini anaweza kufanya kazi zake kwa kuzingatia chama alichokigombea jambo ambalo linaweza likaleta matatizo kwa watumishi wenye imani ya vyama tofauti.
Akizungumzia uwepo wa tume ya kusimamia masuala ya kisekta kama walimu, tume ya elimu na tume ya afya, alisema hoja hiyo wameipokea na imeinginzwa kwenye rasimu ya katiba.
Alisema uwepo wa chombo cha kuzuia na kupambana na rushwa kamati hiyo imepokea pendekezo hilo na sasa chombo hicho kitaanzishwa na kutambulika kikatiba, lakini hata hivyo hakitahusika na masuala ya kushughulikia uhujumu wa uchumi.