Na Fatina Mathias, Dodoma
BENKI ya NMB imetoa msaada wa shilingi milioni 10 kwa ajili ya skuli na hospitali katika kata ya Kibaigwa ikiwa ni jitihada za kuwashukuru wananchi kwa kuendelea kuwaunga katika maendeleo ya kibenki.
Hayo yalibainishwa na Meneja Kanda ya Kati, Gabriel Ole Loibanguti,katika ufunguzi wa tawi jipya la benki hiyo.
“Kwa kutambua nia ya kuendelea kuchagangia huduma mbalimbali, benki ya NMB imetoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili kuchangia maendeleo ya wanachi wa Kibaigwa kama shukrani zetu,” alisema.
Alisema fedha zitakabidhiwa pale uongozi wa benki hiyo utakapokaa na wa wilaya ya Kongwa.
Alisema kabla ya kufunguliwa kwa tawi hilo, wananchi walikuwa wakifuata huduma za kibenki makao makuu ya wilaya Kongwa na wengine kusafiri hadi Dodoma mjini.
Alisema kufunguliwa kwa tawi hilo kunatokana na wananchi na wafanyabiashara wa soko la mahindi Kibaigwa kuhitaji huduma hiyo kutokana na kutembea na fedha zao mkononi na hivyo kuhatarisha maisha yao.
Aidha alisema kufunguliwa kwa tawi hilo, NMB inafikisha jumla ya matawi ya benki hiyo kufikia 150 na zaidi ya mashine 500 za ATM kwa nchi nzima.
Akizindua benki hiyo, Naibu Spika na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai,aliishukuru benki hiyo kwa kutambua umuhimu wa kuwapelekea wananchi huduma hiyo.
Alisema awali usalama wa fedha za wananchi na wafanyabiashara wanaouza mazao na matrekta zilikuwa mashakani kutokana na wezi na majambazi.
Alisema tawi hilo litawasaidia wananchi wa eneo hilo kufaidika na mikopo inayotolewa na benki hiyo jambo ambalo litasaidia kuinua vipato na uchumi wa eneo hilo.
Aliiomba benki hiyo kuwapunguzia wananchi masharti ya mikopo inayotolewa kwao pamoja na riba zinazotozwa ili kujenga uhusiano mzuri kutoka idara hizo.