Na Salim Said Salim
MARA nyingi hujiuliza nini maana ya neno uchochezi na hali ipo vipi katika mtazamo wa viongozi wa Jeshi la Polisi waliopo Zanzibar.
Ninapojiuliza suala hili huibuka masuala mengine zaidi.
Nayo ni pamoja na jee uchochezi hutegemea nani ametamka hilo neno linalotafsiriwa kuwa uchochezi?
Kwa kweli kwa hali inayojitokeza Zanzibar inakuwa vigumu kujua nani anaamua kama kauli liyotamkwa au kitendo kilichofanyika ni cha uchochezi.
Ninapoitafakari hali hii huona mtu hatakosea akiamini wenye uwezo, ustadi na ubingwa wa kuamua kauli gani au kitendo kipi ni cha uchochezi ni viongozi wa CCM.
Hii labda inatokana na ustadi na mapenzi makubwa ya nchi ya viongozi hawa wa CCM ndiyo maana siku zote utaona Jeshi la Polisi linafuatilia kwa makini maelekezo yao.
Mara tu baada ya viongozi wa CCM wakimtangaza mtu kuwa mchochezi na kulitaka Jeshi la Polisi limshughulikie ipasavyo utaona wakuu wa Jeshi la Polisi wanahangaika kumtafuta huyo aliyeitwa mchochezi.
Hiyo ndiyo taswira iliyojengeka Visiwani ukifuatlia msururu wa matokeo ya muda mrefu hivi sasa.
Jingine la ajabu ni kwamba siku zote wachochezi ni viongozi wa upinzani au wale wa dini ambao mawazo yao yanatofautiana na viongozi wa CCM.
Katika kizungumkuti hiki kisichotofautiana na ule mchezo watoto wanapotaka kuanza kucheza chandimu kwa kupiga ndiki, ndikiki, utasikia kwanza anachomoza kiongozi wa CCM akiwa na hasira kuonesha ni mpenda amani na utulivu na mwenye uchungu mkubwa nchi hii.
Kiongozi huyo huanza kwa kumnyooshea mtu kidole kuwa mchochezi na kutaka polisi wamshughulikie.
Lakini wakati huo huo kiongozi huyo wa CCM hujifanya hana habari ya jinsi viongozi wenzake wanavyotukana watu katika mikutano ya hadhara, kama vile matusi hayahatarishi amani ya nchi.
Je, hata mabango ya maskani ya CCM yanayozungumzia masuala mbali mbali kwa lugha ya ufedhuli na uhuni pia si uchochezi?
Ukishasikia tuhuma hizo kutoka kwa viongozi wa CCM Jeshi la Polisi husonga mbele na kueleza kwamba wanamsaka huyo aliyeitwa mchochezi ili kumfungulia mashitaka.
Hapo tena zitapita siku, wiki, miezi na hata mwaka na kitachosikika ni kuwa polisi wapo mbioni kukamilisha upelelezi na anayeshutumiwa huwekwa mahabusu.
Kauli ya Rais mstaafu Komandoo Salmin Amour kuweka mtu mahabusu kwa muda mrefu hakuna matatizo kwa vile mtu si papai na hataoza akiwa gerezani.
Wakati watu hawa wakisota gerezani kwa kukosa dhamana na kusikika madai ya ukikukwaji wa haki za binadamu umma huambiwa mahakama za Zanzibar ni huru na hazitiwi shemere na taasisi za kutetea haki za binadamu au magazeti.
Hali kama hii imetokea karibuni baada ya ziara ya kiongozi wa dini ya Kiislamu kutoka Dar es Salaam, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Kiongozi mmoja wa CCM alisikika kupitia kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) akidai Ponda alifanya uchochezi na kutaka polisi wamkamate.
Haukupita muda, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa, akitangaza kwamba kitengo cha upelelezi kilikuwa kinamsaka Sheikh Ponda kwa kuendesha mihadhara ya uchochezi inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano kwa wananchi Visiwani humu.
Hata hivyo, Kamishna Musa ,alikataa kwamba uamuzi huo haukutokana na shinikizo za viongozi wa CCM na kueleza kuwa hapo kabla walikuwa wanaifanyia kazi kauli hiyo kimya kimya.
Kama kazi hiyo ilikuwa inafanywa kimya kimya nini basi kiliwekwa hadharani?
Inawezekana ni kweli Jeshi la Polisi lilikuwa linaifanya kazi, lakini namna hali ilivyojitokeza, kama siku za nyuma, mwenendo huu unatia mashaka.
Jeshi la Polisi siku zote limekuwa likitueleza kwamba haliendeshwi na amri za wana siasa, bali linaongozwa na sheria za nchi, lakini mwenendo wake ndio unaozusha mashaka.
Baya zaidi ni kwamba pamekuwepo na malalamiko mengi juu ya jeuri za baadhi ya wana siasa wa CCM katika mikutano ya hadhara, lakini hapasikiki habari za kudadisiwa juu ya kauli hizo za matusi.
Mabao yenye matusi yapo hadharani kwa wapiti njia kusoma na wanaoandika hawaguswi na wahusika hawaonywi kuacha mwenendo huu. Si ajabu tukaambiwa polisi hawana taarifa hizo.
Mapema mwaka huu paligawiwa vikaratasi vyenye maneno machafu dhidi ya marais wastaafu wa Muungano, Benjamin Mkapa na wa Zanzibar, Amani Abeid Karume. Mpaka leo hatujasikia mtu yeyote kudadisiwa kuhusu vikaratasi vile vyenye matusi au kama palifanyika uchunguzi kuwajua nani walisambaza uchafu ule.
Wakati umefika kwa Jeshi la Polisi kujiweka katikati ili jamii ione halifanyi ubaguzi wa aina yoyote ile kwa zile zinazoitwa kauli za uchochezi.
Vile vile suala la dhamana lionekane kuwa ni haki ya mshitakiwa, ijapokuwa ni kweli binadamu si papai kuwa ataoza gerezani, lakini kitendo cha kumuweka mtu muda mrefu mahabusu kwa maelezo kuwa upelelezi unaendelea hakitoi sura ya haki kutendeka.
Katika sheria tunaambiwa kwamba hata haki ikikawia kutolewa basi huwa sawa na kutoitoa kabisa.
Siku hizi katika nchi nyingi mtu hufunguliwa mashitaka baada ya kukamilika upelelezi na kuonekana kuwepo ushahidi wa shutuma zinazomkabili na si kumkamata kwanza na kuchukua muda mrefu kufanya upelelezi.
Mwenendo unaoonekana wa kuwafanya viongozi wa CCM kama malaika, hivyo hawana makosa na wengine ndio wanaotenda makosa hautoi taswira nzuri kwa Jeshi letu la Polisi.
Wanaohusika inafaa kuliangalia suala hili, yaani kwa sababu hautoi sura nzuri hapa nchini na nje.
Matokeo yake ni kwa jamii kupoteza imani na Jeshi la Polisi na kuliona limejikita zaidi kufanya kazi kisiasa badala ya kufuata mstari wa sheria. Siku zote wanaofikishwa mahakamani ni viongozi wa kambi za upinzani na wale ambao mawazo yao yanapinga msimamo wa serikali katika masuala mbali mbali.
Kutoa mawazo tofauti ni haki ya raia na hii lazima iheshimiwe. Kwa mfano, kama viongozi wa CCM wanawaona wanaotaka nchi iwe na mfumo wa serikali tatu ni wasaliti, wale wanaotaka kuendelea na serikali mbili ni wasaliti pia, wanayo haki ya kutoa mawazo hayo.
Kutofautiana ndiyo demokrasia. Hizi si zama za kutiana shemere na kutaka watu wote wawe na mawazo ya aina moja. Zama za kutishana zimepita na umma haupo tayari kuridhia.
Mahakama nazo zichukue mkondo wake ili ziwe huru na kwa njia hiyo tu ndiyo tutajenga demokrasia ya kweli. Tubadilike, wakati unatukimbia
Chanzo - Tanzania Daima
Chanzo - Tanzania Daima