TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAKAMU WA RAIS AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA KONGAMANO LA PILI LA KIMATAIFA LA BIASHARA KWA NCHI ZA AFRIKA JIJINI DUBAI
OKTOBA 03, 2014
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Oktoba Mosi, 2014 ameiwakilisha Tanzania katika kongamano la pili la Kimataifa la Biashara kwa nchi za Afrika lililofanyika katika jiji la Dubai, Falme za Kiarabu.
Kongamano hili limehudhuriwa na washiriki wapatao 800 kutoka nchi mbalimbali duniani na limelenga katika kukuza uwekezaji katika nchi za Falme za Kiarabu na kufungua fursa za kibiashara barani Afrika. Kongamano la kwanza la namna hii lilifanyika pia jijini hapa mwaka jana na kushirikisha washiriki wapatao 3000 kutoka nchi mbalimbali duniani.
Baadhi ya Viongozi wa Afrika waliohudhuria kongamano hilo ni pamoja na Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais John Dramani Mahama wa Ghana na Rais Mulatu Teshone Watu wa Ethiopia.
Viongozi hawa kwa nyakati tofauti walizungumzia umuhimu wa utengamano barani Afrika na wakaeleza kuwa hiyo ndiyo fimbo pekee ya kukuza uwekezaji wenye tija Afrika.
Pia walizungumzia mabadiliko makubwa ya Afrika huku wakiwakumbusha wawekezaji na wafanyabiashara waliohudhuria kongamano hilo kuwa Afrika ya sasa siyo bara la giza na kwamba ni bara linalokuwa kimaendeleo kwa kasi huku likiwa na fursa ya kukuza maendeleo yake kwa haraka. Kongamano hili pia lilihudhuriwa na Mfalme Sheikh Mohammed Bin Rashid Al-Makhtoum ambaye alialikwa na wenyeji wa kongamano hili yaani Kituo cha Biashara cha Dubai. Sambamba na hao pia kulikuwa na wafanyabiashara wakubwa akiwemo Aliko Dangote, ambaye sambamba na kuwa na uwekezaji mkubwa katika Afrika pia anawekeza mkoani Mtwara katika ujenzi wa kiwanda kikubwa cha simenti kuliko vyote Afrika Mashariki.
Mfanyabiashara huyo mara baada ya mijadala ya ufunguzi wa kongamano hilo, pia alipata nafasi ya kukutana na mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal na kubadilishana naye mawazo kuhusu uwekezaji wake Tanzania ambapo aligusia nia ya kutumia mkaa wa mawe uliopo Mbinga katika uzalishaji wa nishati kiwandani kwake pamoja na kutanua sekta ya usafirishaji ili kumudu kusafirisha saruji kwa matumizi ya nje ya nchi.
Mfanyabiashara huyo alifafanua kuwa, katika sekta ya usafirishaji pekee anatarajia kuchangia ajira zipatazo 3000 na pia anakusudia kuwapa mafunzo wafanyakazi wa kiwanda chake nchini Nigeria ili waendane na teknolojia ya sasa katika uzalishaji.
Uwekezaji wa Aliko Dangote katika Tanzania unatokana na nchi yetu kuwa na sera nzuri za uwekezaji na anafafanua kuwa maendeleo ya ujenzi wa kiwanda chake yanakwenda kama alivyopanga na ujenzi utakapokamilika na uzalishaji kuanza, ni wazi eneo la Kusini mwa Tanzania litaanza kubadilika kiuchumi kufuatia uwekezaji huo mkubwa.
Mheshimiwa Makamu wa Rais akichangia katika mjadala ambao pia ulimshirikisha Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Balozi Richard Sezibera, alisema nchi za Afrika na hususani Tanzania zimepiga hatua katika kuweka mazingira ya uwekezaji licha ya kuwa changamoto ya uduni wa miundombinu na urasimu. Mheshimiwa Makamu wa Rais alisema, Tanzania imeunganika katika mtandao wa barabara hivyo kwa wawekezaji ni rahisi kwao kuwekeza huku pia nchi yetu inategemea kuwa na ziada ya umeme katika miaka michache ijayo hali itakayohakikishia uhakika katika uzalishaji hasa wa viwanda vikubwa vinavyohitaji nishati kubwa ya umeme ili kuzalisha.
Pia alisisitiza kuhusu umuhimu wa nchi za Afrika kuungana ili kurahisisha matumizi ya miundombinu sambamba na kutanua masoko katika nchi za Afrika na akaeleza kuwa Tanzania iko mstari wa mbele kuhakikisha inachangia uwezo wake katika kuhamasisha nchi kuungana kwa lengo la kukuza mahusiano, kuimarisha amani na kutanua fursa za uwekezaji.
“Sisi Tanzania tupo katika uhusiano na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki sambamba na zile za Kusini mwa Afrika. Ushiriki wetu katika jumuiya hizi unasaidia pia hasa sasa ambapo tunazungumzia kuweka mashirikiano na nchi za Magharibi ya Afrika na hivyo kuwa na mfumo mmoja wa biashara barani Afrika,” Mheshimiwa Makamu wa Rais anasisitiza.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Makamu wa Rais alikutana na Makamu wa Rais wa Sychelles Mheshimiwa Danny Faure ambaye alimuelezea Mheshimiwa Dkt Bilal kuwa, Sychelles inakusudia kuanza safari ya ndege zake kuleta watalii Tanzania sambamba na kununua mazao ya kilimo na ufugaji na hivyo kuwa fursa mpya kwa wakulima wa mbogamboga, vitunguu na wafugaji wa ng’ombe.
Mheshimiwa Faure alimueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, uhusiano baina ya Tanzania ni Sychelles ni mkubwa na hivyo ili kuuwekea msingi imara upo umuhimu wa kushirikiana katika biashara hasa kwa bidhaa ambazo hazipatikani Sychellles.
Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal alipokea taarifa hiyo na kumueleza Makamu wa Rais Faure kuwa, Tanzania itatoa taarifa kwa wafanyabiashara wake ili waweze kuchangamkia fursa hiyo kupitia Bodi ya Biashara za Nje (Tantrade).
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Oktoba 3, 2014 Dubai, UAE