HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA
MAPINDUZI, MHESHIMIWA AL-HAJ DK ALI MOHAMED SHEIN,
KATIKA BARAZA LA IDD EL HAJJ, OKTOBA, 2014
(Mwezi 10 Mfunguo Tatu: 1435)
Bismillahi Rahmani Rahim,
Shukurani zote anastahiki Mwenyezi Mungu Mtukufu; Mola wa viumbe wote. Mwenyezi Mungu ndiye anayestahiki kukusudiwa na viumbe wote kwa kumuabudu, kumuomba msamaha na kumtegemea.
Sala na salam zimshukie Mtukufu wa daraja, Mtume wetu na kigezo chetu; Nabii wa Mwenyezi Mungu, Sayyidna Muhammad (S.A.W) pamoja na wafuasi wake wote hadi kitakaposimama kiama. Mwenyezi Mungu atujaalie na sisi tuwe miongoni mwa wenye kufuata mwenendo wao na kupata malipo mema hapa duniani na huko akhera twendako. AMIN!
Ndugu Wananchi,
Mheshimiwa Sheikh Khamis Haji Khamis;
Kadhi Mkuu wa Zanzibar,
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad;
Makamu wa Kwanza wa Rais,
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi;
Makamu wa Pili wa Rais,
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho;
Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Mheshimiwa Omar Othman Makungu;
Jaji Mkuu wa Zanzibar,
Waheshimiwa Mawaziri,
Waheshimiwa Mabalozi,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Assalamu Aleikum Warahmatullah Wabarakatuh
IDD MUBARAK
Nimeanza kwa kushuhudia kuwa hapana Mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah (SW) na kumsalia mbora wa waja; Mtume wetu Seyyidna Muhammad (S.A.W) pamoja na wafuasi wake. Hapana shaka ni uwezo wake Subhana Wataala kutujaalia neema ya uhai tukaweza kuidiriki siku hii na kuiadhimisha kwa Takbira nyingi.
Kwa mapenzi yake Mola wetu kwetu, tumeweza kuungana na Waislamu wenzetu walioko katika Mji Mtukufu wa Makka wanaoendelea kutekeleza Ibada ya Hija ambayo ni nguzo ya tano ya Uislamu. Waislamu wa Zanzibar na Tanzania nzima kwa jumla tunaungana na wenzetu duniani kote kumuomba Mwenyezi Mungu awatakabalie ibada zao zote, awawezeshe kuzingatia mafunzo ya Hija na kuyaendeleza na awarudishe nyumbani salama ili waweze kuungana tena na familia, jamaa, marafiki na wananchi wenzao.
Ndugu Wananchi,
Mwenyezi Mungu ametujaalia Waislamu sikukuu mbili kubwa kila mwaka; Sikukuu ya Idd el Fitri na Sikukuu ya Idd el Hajj, tunayoisherehekea leo. Miezi miwili iliyopita na siku kidogo, tulisherehekea Sikukuu ya Idd el Fitri baada ya kuikamilisha ibada ya swaumu katika mwezi Mtukufu wa Ramadhan na leo tena tupo hapa Micheweni katika Chuo cha Kiislamu hapa Kiuyu kwa ajili ya Sikukuu ya Idd Al- Adhha, ambayo tunasali Idd na kuchinja kama ilivyoagizwa katika Suratul Kawthar, aya ya kwanza na ya pili zenye tafsiri isemayo:
“Hakika tumekupa kheri nyingi”.
“Basi sali kwa ajili ya Mola wako na uchinje”.
Mbali na wajibu wetu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuzifikia sikukuu hizi tukiwa hai, vile vile, tuna wajibu wa kuzingatia mafunzo yanayotokana na ibada hizi na kuyaendeleza katika maisha yetu ya kila siku hapa duniani.
Ndugu Wananchi,
Ibada ya Hija imekusanya mambo mengi yanayomkurubisha mja kwa Mola wake. Hija ni mithili ya taasisi ya mafunzo ya malezi na maarifa kwa Waislamu katika misingi ya tawhidi kwa kumtukuza Mwenyezi Mungu na huanza kwa kuweka nia safi na ikhlasi. Mafunzo haya yana mchango muhimu kwa mja kuwa mcha Mungu kwa kujiepusha na vitendo vyote vitakavyomtoa katika njia ya Mwenyezi Mungu na mafunzo ya Bwana Mtume Muhammad (SAW) aliyeletwa kwetu kutupa miongozo.
Mwenyezi Mungu anatukumbusha kwenye Kurani katika sehemu ya aya ya 7 ya Suratul Hashir yenye tafsiri isemayo:
“…… Na anachokupeni Mtume basi pokeeni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho. Na muogopeni Mwenyezi Mungu; kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu“.
Kwa mnasaba wa aya hii, Mwenyezi Mungu anatuasa kuzingatia mafunzo ya Bwana Mtume kwa kufanya yote tuliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu (SW), likiwemo hili la kutekeleza ibada ya Hija na kuzingatia mafunzo yake na kutubainishia ubaya wa kushindwa kuitekeleza kwa wale waliojaaliwa kuwa na uwezo. Mtakumbuka katika hotuba yangu ya Idd el Fitri nilieleza kuwa mafunzo ya Saumu ya Ramadhani ni mfano wa mafunzo ya Chuo Kikuu. Mafunzo yanayohusiana na utekelezaji wa Ibada ya Hija nayo ni mafunzo ya daraja la juu. Mwenye kufuzu na kupata hio daraja ya juu, kwa hakika hupata fadhila kubwa kwa Mwenyezi Mungu, hadhi na heshima hata ya kumtambua kuwa Al-Hajj kwa mwanamme na Hajjat kwa mwanamke.
Kwa hivyo, tunapaswa kuwapongeza Waislamu wenzetu waliofanikiwa kwenda kuitekeleza ibada ya Hija na tuwape heshima wanayostahiki. Pamoja na hayo, tuzidi kuwaombea hija zao zikubaliwe. Wale watakaofuzu huwa wamefutiwa madhambi yao yote, kama inavyosema hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Sayyidna Abu Huraira (RA), Bwana Mtume (S.A.W) amesema:
“Mwenye kufanya Hijja bila ya kusema maneno machafu na bila ya kufanya vitendo vichafu, atasamehewa madhambi yake arudi kama siku aliyozaliwa na mama yake”
Tumuombe Mola wetu (SW) azikubali ibada za Waislamu wenzetu wote waliokwenda kuitikia wito Wake wa kwenda kufanya ibada hiyo.
Ndugu Wananchi,
Jambo jengine muhimu tunalojifunza katika Ibada ya Hija ni kubainisha hisia za Umoja wa Kiislamu na usawa wa wanaadamu mbele ya Mwenyezi Mungu. Waislamu kutoka mataifa mbali mbali, wenye nyadhifa, uwezo na rangi mbali mbali hukusanyika pamoja katika mji mtukufu wa Makka na Madina, wakiwa na lengo moja la kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu wa kufanya ibada katika nyumba tukufu ili kupata uongofu. Katika Surat Al- Imran aya ya 96 Mwenyezi Mungu amesema,
“Kwa yakini Nyumba ya kwanza iliyowekwa kwa ajili ya watu (kufanya ibada) ni ile iliyoko Makka, yenye baraka na yenye uwongofu kwa ajili ya walimwengu wote”.
Na katika aya ya 97 ya Sura hiyo Mwenyezi Mungu ameendelea kusema:
“Humo mna ishara zilizo wazi (za kuonesha utukufu wake na ukongwe wake. Miongoni mwa hizo ni) mahali alipokuwa akisimama Ibrahimu, na anayeingia (nchi hiyo) anakuwa katika salama. Na Mwenyezi Mungu amewawajibishia watu wafanye Hija katika Nyumba hiyo, yule awezaye kufunga safari kwenda huko .……”.
Ni faraja iliyoje kwa Muislamu kupata wasaa katika uhai wake kujumuika katika mkusanyiko mkubwa wa Umoja wa Waislamu wa kila mwaka katika nyumba tukufu. Katika mazingira haya mahujaji hupata fursa ya kujadiliana masuala mbali mbali ya kuuendeleza Uislamu na kuzifanyia kazi changamoto zinazowakabili katika ulimwengu wa leo. Kadhalika, mkusanyiko huu ni kielelezo cha umoja, udugu na mshikamano wa Waislamu kwamba wanafuata miongozo ya Kurani Tukufu na Hadithi za Bwana Mtume Muhammad (S.A.W).
Ndugu Wananchi,
Hapana shaka kwamba maarifa mapya wanayoyapata mahujaji wetu wanapofanya ibada ya Hija, yatakuwa na manufaa zaidi iwapo watakuja kuyaendeleza watakaporudi hapa nyumbani. Ni dhahiri kuwa nchi yetu inahitaji sana kuzidi kuendelezwa kwa hali ya umoja na mshikamano wetu kwani ndio siri kubwa ya mafanikio tuliyoyapata katika kuimarisha amani tuliyonayo, ustawi wa uchumi na kukuza maendeleo ya jamii.
Kwa hivyo, kwa kuwa hali hiyo ya umoja na mshikamano, mtu anaweza kuihisi katika wiki chache tu za kukutana na watu kutoka nchi mbali mbali kwa mamilioni wakati wa Hija, ni vyema akaiendeleza wakati anaporudi hapa nyumbani tunapoishi siku zote. Hiyo itakuwa ndiyo namna bora ya kuyatumia mafunzo hayo yanayotakiwa yadumu katika maisha yetu ya kila siku na ndio kielelezo bora cha mtu aliyekwishahiji.
Ndugu Wananchi,
Vile vile, mahujaji wetu hunufaika katika kuziimarisha imani zao kutokana na kuyatembelea maeneo mashuhuri ya historia ya Uislamu, wakiwa na amani ya nafsi na ya kimazingira wakati wote. Katika kipindi chote cha Hija ndugu zetu hawa huwa ni wageni wa Mwenyezi Mungu Mkarimu. Katika hadithi iliyopokelewa na Sayyidna Anas bin Malik (RA), Bwana Mtume (S.A.W) amesema:
“Mwenye kufanya Hija na mwenye kufanya Umra ni wageni wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hupewa wanachoomba, na (Allah) anajibu dua zao, na hurudishiwa walivyotoa, dirham (au shilingi) moja kwa dirham (au shilingi) milioni moja” (Al baihaqiy).
Katika hadithi nyengine iliyopokelewa na yeye Sayyidna Anas bin Malik (RA) vile vile Bwana Mtume (S.A.W) amesema:
Kutoa kwa ajili ya Hijja ni sawa sawa na kutoa kwa ajili ya jihad; dirham moja kwa mia saba” (Tabrany)
Riwaya hii imetafsiriwa na baadhi ya Maimamu kuwa inamaanisha kwamba hata wale wasiokwenda Hija, lakini kwa namna mbali mbali hushiriki katika kuwaandalia safari Mahujaji wetu, vile vile nao Mwenyezi Mungu huwalipa malipo makubwa. Napenda kutoa shukurani zangu kwa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, kwa kushirikiana vyema na taasisi zote zilizohusika katika kuwasafirisha Mahujaji wetu kwa kuwahudumia vyema tangu mwanzo hadi sasa na Inshaallah mpaka hapo watakaporudi hapa nyumbani. Tumuombe Mwenyezi Mungu sote atupe ilham, afya na uwezo wa kupata kuitekeleza nguzo hii ya tano ya Kiislamu na kuwasaidia kwa kila namna wenzetu waliojaaliwa uwezo wa kwenda kuhiji ili sote tuweze kunufaika na fadhila zake.
Ndugu Wananchi,
Napenda kutumia fursa hii kusisitiza umuhimu wa kuyaendeleza mafunzo yanayotokana na ibada zetu mbali mbali katika maisha yetu ya kawaida, hasa suala la kuhimizana kufanya mambo mema na kukatazana mambo mabaya. Kufanya hivyo ni kuitii amri ya Mola wetu Mtukufu, kutekeleza mafundisho wa Bwana Mtume (S.A.W) pamoja na jamii inayozingatia misingi ya sheria na utawala bora.
Mwenyezi Mungu huongeza baraka na neema katika jamii ambayo huzishukuru neema zake kwa kuzitumia katika njia inayolenga kunufaisha watu walio wengi.
Kwa kutumia uwezo wa rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu ametujaaliya nchini, Serikali inaendelea na jitihada zake kwa kushirikiana na washirika wetu wa maendeleo mbali mbali katika kuimarisha miundombinu ikiwemo barabara, usambazaji wa maji safi na salama, huduma za umeme na mengineyo.
Katika Mkoa huu wa Kaskazini Pemba, wenyeji wa Mkoa huu na hata baadhi ya wageni ni mashahidi wa kubainisha jitihada hizo ambazo naamini matunda yake yanafurahiwa na watu wengi kwani mambo haya ya maendeleo yaliofanywa ni ukombozi mkubwa wa hali ya maisha ya wananchi.
Serikali kwa kushirikiana na washirika wetu wa maendeleo imefanya juhudi kubwa ya kuimarisha miundombinu ya barabara katika Mkoa huu. Ni dhahiri kuwa, kuimarika kwa miundombinu ya barabara kutasaidia sana katika kuimarisha sekta nyingine za kiuchumi.
Kwa kipindi kirefu miundombinu ya barabara ilikuwa ni changamoto kubwa kwa wananchi kwa ajili ya kuendesha maisha yao na kwa wawekezeji wengi waliokuwa na azma ya kuwekeza katika katika sehemu mbali mbali nchini. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitangaza maeneo huru ya uchumi katika mwaka 1992, ambapo ilitenga eneo la Fumba kwa upande wa Unguja na eneo la Micheweni kwa upande wa Pemba; kwa ajili ya kazi hiyo. Ukosefu wa miundombinu ya barabara za kisasa kwa kipindi kirefu ulikwamisha jitihada zetu za kupata wawekezaji wenye viwango tunavyotaka katika maeneo huru yaliyotengwa hapa Micheweni na Mkoa wa Kaskazini, Pemba kwa jumla. Ni dhahiri kuwa, hatua tuliyofikia hivi sasa ya kuimarisha miundombinu, itasaidia sana katika juhudi zetu za kutafuta wewekezaji tunaowataka.
Ndugu Wananchi,
Kwa bahati mbaya, wapo baadhi ya wananchi wachache ambao wanaendelea kuweka mbele maslahi yao kwa kuharibu maslahi ya wengi. Katika maeneo mengi ya Unguja na Pemba kumekuwa na uharibifu wa makusudi wa miundombinu mbali mbali, licha ya Serikali kutumia fedha nyingi katika kuiimarisha. Wapo baadhi ya watu wanaong’oa nguzo na mabati ya alama za barabarani. Kwa upande wa miundombinu ya umeme, wako wanaokata nyaya za transforma. Kesi za uharibifu wa transforma ni nyingi ikiwemo iliyotokezea mwezi Agosti, mwaka huu katika eneo la Mwembe Shauri, Unguja na kesi nyengine kwenye visima vya maji. Kadhalika, funiko za chuma za makaro kwenye maeneo ya miji zinachukuliwa na kuuzwa kama vyuma chakavu. Mambo haya hayatoi taswira nzuri katika jamii yetu. Kwa hivyo, sote tunapaswa tushirikiane ili tuweze kuvizuwia vitendo hivi kwani, vina athari kubwa kwa ustawi wa maendeleo yetu.
Ndugu Wananchi,
Wakati huu tunaposherehekea sikukuu hii ya Idd el Hajj tunaendelea na msimu wa mavuno ya karafuu katika mwaka 2014/2015 tuliouanza mwezi Julai, 2014. Hatuna budi tumshukuru Mwenyezi Mungu (SW) kwa kutujaalia neema hii kubwa. Kadhalika, napenda kutoa shukurani za dhati kwa wakulima wote wa karafuu nchini kwa kuendelea kuziuza karafuu zao katika vituo vya Shirika letu la ZSTC. Nimearifiwa kuwa hadi kufikia tarehe 2 Oktoba 2014 tani 1,347.65 za karafuu zenye thamani ya Tsh.Milioni 18,862.7 zimeshanunuliwa katika vituo vyetu vya ZSTC Unguja na Pemba. Haya ni mafanikio ya kutia moyo.
Serikali imejiandaa vyema kuhakikisha kuwa karafuu zote zinanunuliwa pamoja na kuhakikisha kwamba wakulima wa karafuu wanapata vifaa vyote wanavyohitaji katika shughuli zao. Aidha, kwa kushirikiana na vikosi vyetu vya ulinzi na usalama tutaendelea kupambana na magendo ya karafuu, ili faida inayopatikana kutokana na zao hili iendelee kuwanufaisha wakulima wetu na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Kwa kuzingatia hali halisi ya bei ya karafuu katika soko la dunia, Serikali haikuweza kupandisha bei ya karafuu kwa msimu huu wa mwaka 2014, lakini imefanya kila jitihada kuhakikisha kuwa bei inabakia kama ilivyokuwa katika msimu uliotangulia wa mwaka 2013/2014 ili kuwapa nguvu wakulima. Siku ya tarehe 9 Julai, 2014 nilipozindua rasmi Msimu wa Karafuu wa mwaka 2014/2015 Serikali ilitangaza bei mpya ya karafuu kuwa kilo moja ya karafuu ya gredi ya kwanza kuwa ni TShs. 14,000 na gredi ya pili kuwa TShs. 12,000 na TShs. 10,000 kwa gredi ya tatu. Nimearifiwa kwamba kumekuwa na mwamko mkubwa kwa wakulima katika kuutunza na kuimarisha ubora wa karafuu zetu, jambo hili limewawezesha wakulima kupata gredi ya kwanza kwa karafuu nyingi wanazoziuza na kuinua kipato chao. Nawapongeza wakulima kwa kuwa na mwamko huu.
Kadhalika, nachukua fursa hii kwa mara nyengine, kuwataka wale wenye tabia ya kuanika karafuu kwenye barabara au kutumia njia mbaya za uanikaji na ukaushaji wa karafuu kuacha tabia hiyo, kwa kuwa ina athari kubwa katika kupata bei bora ya karafuu zetu katika soko la dunia ambalo hivi sasa limejaa ushindani mkubwa.
Katika jitihada za kulinda hadhi na sifa pekee za karafuu zetu, Serikali inakamilisha utekelezaji wa mpango wa kuzipa karafuu za Zanzibar utambulisho maalum (Branding).
Vile vile, Serikali inaendelea kutekeleza ahadi ya kuimarisha miundombinu ya barabara katika maeneo ambayo wakulima wanapata usumbufu kuyafikia mashamba yao ya mikarafuu. Serikali tayari imeshatekeleza ahadi ya ujenzi wa barabara ya Kuyuni – Ngomeni kwa kiwango cha kifusi yenye urefu wa kilomita 3.1. Ujenzi wa barabara hii umegharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mfuko wa Barabara. Hivi sasa tunakamilisha mipango ya kuanza ujenzi wa barabara ya Kipapo-Mgelema pamoja na barabara ya Mgagadu – Kwa Utao. Lengo la Serikali ni kuzijenga barabara hizi kwa kiwango cha lami hapo baadae tutakapopata uwezo. Kumalizika kwa barabara hizo kutarahisisha vile vile utekelezaji wa shughuli nyengine za maendeleo kwa wananchi wa maeneo hayo.
Jitihada za Serikali za kurudisha hadhi ya zao la karafuu zimesaidia sana katika kuinua hali za maisha ya wakulima katika sehemu mbali mbali hasa hapa Pemba. Zao la karafuu limechangia sana kuimarisha mzunguko wa fedha ambao umekuwa ukisaidia sana kuimarisha biashara na shughuli mbali mbali za kiuchumi.
Kwa mara nyengine tena, napenda kuwanasihi wakulima wetu wa karafuu waendelee na jitihada zao za kutumia huduma za benki kwa kuhifadhia fedha zao na kujiwekea akiba. Uamuzi wao huo ni uamuzi wa kimaendeleo. Wale ambao bado hawajachukua hatua, ni busara wakafanya uamuzi huo hivi sasa.
Ndugu Wananchi,
Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya mvua ambayo tumeanza kuipata katika maeneo mbali mbali nchini. Ni vyema tukaitumia neema hii anayoendelea kuturuzuku Mola wetu katika kuimarisha shughuli zetu za kilimo. Tuzitumie mvua hizi kwa kupanda kwa wingi miti ya matunda, mboga mboga, mimea ya vyakula vya mizizi na miti ya misitu na biashara.
Aidha, tuutumie wakati huu kwa kuendeleza kilimo cha mikarafuu kwa kuyashughulikia ipasavyo mashamba yetu. Nimeelezwa kuwa idadi ya miche ya mikarafuu 686,854 itatolewa kwa wakulima katika msimu wa mvua za Masika wa mwaka 2014/2015, ambapo miche 499,354 iliyoatikwa kwenye vitalu vya Serikali na miche 187,500 iliyoatikwa kwenye vitalu vya watu binafsi. Natoa wito kwa wakulima wayatayarishe vyema mashamba yao kwa mujibu wa maelekezo ya wataalamu wa kilimo na misitu, ili juhudi zetu ziweze kuwa na tija zaidi. Tusiusahau msemo mashuhuri wa walimu wetu kwamba “Jitihada ndiyo ufunguo wa mafanikio”. Kwa hivyo, tuzitumie fursa zote zilizopo ili kuliendeleza zao la karafuu ambalo ni tegemeo kubwa kwa uchumi wetu.
Ndugu Wananchi,
Sote tunafahamu kwamba Hija ya mwaka huu kama zilivyokuwa Hija za miaka iliyopita, imekuja wakati dunia yetu ikiendelea kukumbwa na matatizo mbali mbali. Matatizo hayo yanatokana na sababu mbali mbali za uwezo wa Mwenyezi Mungu na zikiwemo zinazosababishwa na binadamu. Matukio ya vimbunga, matetemeko ya ardhi, kuripuka kwa volcano, mabadiliko ya tabianchi, na kadhalika, yameleta athari kubwa pamoja na kupoteza maisha ya watu mbali mbali na mali zao. Aidha, yapo maafa mengine ya maradhi thakili yanayoendelea kuikumba dunia yakiwemo maradhi ya UKIMWI, Ebola na mengineyo.
Nchi yetu inaendelea kukumbwa na maafa kadhaa zikiwemo ajali mbali mbali, hasa za barabarani, athari ya mabadiliko ya tabianchi, kama vile maeneo ya kilimo kuvamiwa na maji ya bahari na visima vya asili vimeingia maji ya chumvi. Jumla ya maeneo 145 yameathirika kwa kuingia maji ya chumvi. Kati ya maeneo hayo, maeneo 123 yapo hapa Pemba.
Tatizo jengine ni kupanda kwa kina cha maji ya bahari duniani kwa maeneo yaliyo chini ya mita tano kutoka usawa wa bahari. Maeneo hayo yapo kwenye hatari ya kuathirika zaidi kutokana na hali hiyo. Kwa upande wa Pemba maeneo ya aina hii yana ukubwa wa mita za mraba 286 na yanakaliwa na asilimia 54 ya watu na kwa Unguja yana ukubwa wa mita za mraba 328 na yanakaliwa na asilimia 29 ya watu. Kadhalika, tunashuhudia namna misimu ya mvua inavyobadilika. Baadhi ya wakati mvua zinachelewa kunyesha na zinapokuja kiwango chake hupungua au hunyesha kwa kiwango kikubwa sana. Upepo unaovuma nao hautabiriki. Pepo za Kusi na Kaskazi, nazo huvuma tafauti na viwango vilivyozoweleka miaka ya nyuma.
Matatizo ya uchafuzi wa mazingira mengine tunayasababisha sisi wenyewe. Suala la utupaji taka ovyo, bidhaa chakavu za kemikali na mifuko ya plastiki pamoja na uchimbaji wa mchanga na mawe madhara yake ni makubwa na lazima tuhakikishe kwamba sheria inasimamiwa vizuri. Aidha, hatuna budi tuendelee kuchukua hatua madhubuti kwa mujibu wa sheria kuzuia ujenzi kwenye vyanzo vya maji na kwenye mabonde yaliyotengwa kwa shughuli za kilimo.
Ndugu Wananchi,
Wapo wananchi, walioathirika na kukabiliwa na shida na matatizo mbali mbali kutokana na maafa yaliyotokea. Serikali zetu mbili, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Jumuiya za Kimataifa na Washirika wetu wa Maendeleo, zinafanya kila jitihada ya kutekeleza mipango yetu na ya Kimataifa katika kukabiliana na maafa. Masuala ya mazingira na tabianchi na yale yote yanayosababisha maafa na majanga katika nchi yetu, yanatekelezwa kwa kuzingatia sera na mipango iliyokwishaandaliwa. Hata hivyo, hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote hayo ambayo ni mitihani yake kwetu. Ni wajibu wetu tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu katika sala zetu ili atulinde na atuepushe na maafa mbali mbali.
Kadhalika, tunapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu atusamehe makosa yetu mbali mbali, ambayo inawezekana mengine yalisababisha baadhi ya maafa, kama vile uharibifu wa mazingira na kadhalika. Tuendelee kumcha na kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa dhati ya imani ya dini yetu kwa kufuata na kuzitekeleza amri zake na mafundisho ya dini tukiwa waumini wa kweli.
Ndugu Wananchi,
Pamoja na kwamba sherehe za leo zinadhihirisha furaha yetu baada ya kukamilika kwa ibada ya Hija, tusisahau kuwa bado maafa yanaweza kutokea wakati wowote na kuikumba jamii yetu. Hali hio inapotokea, sote tunawajibu wa kutoa mchango wetu ikiwa ni pamoja na kuomba dua, ili kukabiliana na hali hio. Kwani dua ndio silaha ya Muumini kama alivyosema Bwana Mtume (SAW).
Kwa hivyo, leo ni fursa nzima ya kujiuliza na kujikumbusha sababu zinazopelekea jamii yetu kukumbwa na mitihani ya Mwenyezi Mungu (SW). Tunafahamu kuwa zipo sababu nyingi zinazofanya mitihani hio itokee na kuikumba jamii yetu.
Imani ya dini inatueleza kwamba binadamu anapofanya maovu na kusahau mafundisho ya dini, kwa hakika anakosa radhi za Mola wake. Sote tunashuhudia kwamba katika jamii yetu siku hizi; vitendo viovu vimekithiri kwa kiasi kikubwa. Baadhi ya vitendo hivyo, ni pamoja na vifo vinavyotokana na ajali za barabarani, mauaji, ubakaji, udhalilishaji wa wanawake na watoto, ujambazi, ulevi, rushwa, dhulma, uhasama na chuki zisizokuwa na msingi, na kadhalika. Kwa hivyo, sote tunakabiliwa na jukumu la kupambana na maovu hayo kwa nguvu zetu zote, ili tuweze kuinusuru jamii yetu na vitendo vinavyotokea kinyume cha maadili yetu.
Ndugu Wananchi,
Jukumu kubwa liko kwetu na kwa viongozi wetu mbali mbali; la kutuhimiza waumini na wananchi, ili tuyawache mambo maovu ambayo ni ya kishetani. Viongozi waendelee daima kukemea maovu katika jamii na kuwahimiza wananchi kuendelea kupendana na kuwasaidia wale wanaostahili misaada, hasa mayatima, walemavu, wazee, maskini na wengine wote wasiojiweza.
Ndugu Wananchi,
Napenda nisisitize kwa mara nyengine tena kuhusu suala la kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu. Nchi yetu imefikia kuwa nchi ya amani kutokana na misingi ya uongozi bora iliyowekwa na viongozi wa awamu zote zilizopita za nchi yetu na uwezo wake Mwenyezi Mungu. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kufurahia baraka alizotupa Mwenyezi Mungu na kufanya kila jitihada ili tuilinde hali hio ya neema na kheri. Ni lazima tuhakikishe kwamba hapana hata mmoja atakayekuwa ni chanzo cha kuvurugika kwa amani katika nchi yetu, kwa visingizio vya harakati za kidini, kisiasa na nyengine zo zote zile. Tuiendeleze sifa ya nchi yetu kuwa ni nchi ya amani kwa kujiepusha na mifarakano na mizozo isiyokuwa na faida yoyote.
Wito wangu ni kwamba ubinafsi usiingie na kupewa nafasi katika masuala yanayohusu jamii, hasa mambo ya siasa na dini. Wale wote wanaofanya hivyo, watambue kuwa wanafanya makosa kwa kufikiri kwamba wana uwezo zaidi kuliko wengine wa kuondosha matatizo katika jamii kwa kutumia nguvu zao. Ni vyema tukaelimishana juu ya mema na mabaya kwa busara, badala ya kiburi na dharau.
Tuendelee kujenga imani yetu na kumuabudu Mwenyezi Mungu hadi mwisho wa uwezo wetu, bila ya kuchoka au kutosheka; ili atukubalie sala na dua za kuitakia nchi yetu iendelee kuwa na amani, umoja, mshikamano na maendeleo.
Tusisahau kamwe kwamba amani na umoja ni misingi ya uhai wa nchi yetu. Waumini na wananchi kwa jumla; hatuna budi kuepuka kushabikia mambo yanayokwenda kinyume na maadili mema. Kwa hivyo, waumini na wananchi wote ni lazima tufanye bidii ya kuendeleza na kuimarisha amani, kwani kwa namna hio tutaendelea kujenga mazingira mazuri yanayofaa kwa waumini kuendelea kufanya ibada na kumcha Mwenyezi Mungu na wananchi sote kujiletea maendeleo yetu. Kwa hivyo, hakuna mbadala katika suala la wa amani. Serikali zetu mbili zitasimamia hali ya amani na utulivu kwa uwezo wetu wote.
Ndugu Wananchi,
Sikukuu ni furaha lakini kila sikukuu huwa na sababu zake kama hii ya leo. Kwa hivyo, tuitumie sikukuu yetu hii kwa kufanya mambo mema yenye mnasaba wa kuonesha furaha na shukurani zetu kwa Mwenyezi Mungu (SW) kwa kutujaalia kuifikia siku hii. Miongoni mwa mambo mema ya kuyatekeleza ni lile la kuchinja mnyama kwa matumizi ya familia zetu na kuwapa sehemu ya mnyama marafiki zetu, mayatima na wenzetu wengine.
Imepokelewa kutoka kwa Abu Rafii (RA) kwamba Bwana Mtume (S.A.W) alikua akichinja kondoo wawili; mmoja kwa ajili yake na familia yake na mwengine kwa ajili ya umma wake. Mambo mengine ya kheri baada ya kusali sala ya Iddi katika siku hii ni kula na kunywa vitu vizuri vya halali, kuvaa vizuri kama tunavyoonekana hapa pamoja na kutembeleana, kupeana zawadi, kuwakagua wagonjwa na kuombeana dua. Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa wafuasi wazuri wa mafundisho na sunna za Mtume wetu (S.A.W) ili tuweze kufanikiwa hapa duniani na kesho akhera.
Napenda kuwanasihi wazazi wenzangu tuendelee kusimamia malezi ya vijana wetu ili nao waige maadili mema na mafundisho ya dini kwa kuziepuka tabia mbaya zisizoendana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu, utamaduni, silka na malezi ya jamii yetu. Tuwasimamie mavazi yao ili tuone kuwa wanavaa mavazi ya stara yaliyo muruwa na wanapokwenda kwenye viwanja vya sikukuu hawajisahau na wanarudi nyumbani mapema na wanayafikia malengo ya sikukuu zetu.
Ndugu Wananchi,
Kama kawaida yangu, nataka nizungumzie umuhimu wa matumizi mazuri ya barabara zetu kwa kuepusha ajali zisizo za lazima hasa katika nyakati hizi za sikukuu. Sheria za usalama barabarani zimekuwa zikivunjwa kwa kupakia abiria na watoto zaidi ya wale wanaokubalika kisheria. Baadhi ya madereva huendesha gari zao kwa mwendo wa kasi, alama za usalama barabarani wanazipuuza na kusababisha ajali ambazo zingeweza kuepukwa iwapo wangekuwa waangalifu.
Taarifa kutoka katika Jeshi la Polisi zinaeleza kuwa kuanzia mwezi wa Januari hadi Agosti mwaka huu wa 2014 kumeripotiwa ajali za barabarani 314 zilizohusisha magari na kusababisha vifo vya watu 53 na majeruhi 377. Matukio yaliyohusisha waendesha vyombo vya moto vya maringi mawili katika kipindi hicho ni 112 na kusababisha vifo vya watu 25 na majeruhi 161.
Katika hali kama hii, lazima Jeshi la Polisi liweke mikakati ya kukabiliana nayo na kushirikiana na taasisi zinazowasimamia madereva na ukaguzi wa vyombo vyao ili kuhakikisha kuwa madereva wanaokiuka sheria na vyombo vya usafiri wa barabarani ambavyo ni vibovu, na haviwi vyanzo vya ajali za barabarani. Wananchi wengi wananung’unika juu ya mwenendo mbaya wa madereva wa magari makubwa yanayobeba mchanga kwa kukosa hadhari barabarani, Unguja na Pemba. Naziagiza taasisi zote zinazohusika kuyafanyia kazi manung’uniko haya ya wananchi na wawachukulie hatua kali za kisheria madereva watakaobainika kuvunja sheria kwa sababu ya ukubwa wa vyombo wanavyoviendesha. Hatuwezi kuwaruhusu madereva wasiojali utu kuendelea kukiuka sheria na kusababisha ajali.
Kadhalika, wananchi waendelee kuelimishwa juu ya masuala ya usalama barabarani na matumizi mazuri ya barabara, ili uzuri wa barabara zetu tunazoendelea kuzijenga ulete faraja kwa wananchi badala ya kusababisha madhara ya kupata ulemavu au kupoteza maisha.
Ndugu Wananchi,
Namalizia hotuba yangu kwa kutoa pongezi na shukurani zangu kwa Kamati ya maandalizi ya sherehe hizi kwa kazi nzuri ambayo sote tumeridhika nayo. Natoa shukurani kwa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana vyema na viongozi mbali mbali wakiwemo Maafisa Wadhamini wote katika kila hatua. Ni dhahiri kuwa kufanikiwa kwa sherehe zetu za leo kumetokana na michango ya kila mmoja wenu. Shukurani zangu za dhati kwa viongozi na wananchi wote wa Mkoa wa Kaskazini Pemba pamoja na wananchi wote wa Pemba kwa mapokezi mazuri na mahudhurio makubwa katika sala ya Iddi leo asubuhi na kwenye Baraza hili la Idd-el-Hajj.
Kwa pamoja tuendelee kuwaombea dua Mahujaji wetu iwe Hijjah Mabrur kwao na Mwenyezi Mungu awarudishe nyumbani kwa salama. Mwenyezi Mungu (SW) atuzidishie amani, umoja na mshikamano ili tuweze kupiga hatua zaidi za maendeleo. Awape afya njema na subira wagonjwa wetu walioko majumbani na hospitalini. Awarehemu wazee wetu na awasamehe makosa yao wote waliokwishatangulia mbele ya haki. Mwenyezi Mungu atupe mvua zenye kheri na baraka na neema ya mazao. Atujaalie sote turudi nyumbani kwa salama na tusherehekee sikukuu hii kwa amani, furaha na utulivu.
Wassalamu Aleikum Warahmatullah Wabarakatuhu
IDD MUBARAK, WAKULLU AAM WAANTUM BIKHEIR
Ahsanteni kwa kunisikiliza.