Na Bakar Mussa, Pemba
Lita 250 za mafuta zenye thamani ya shilingi milioni tano, zimekamatwa na vikosi vya SMZ katika bandari ya Uchungani Wesha mkoa wa kusini Pemba.
Akizungumza na waandishi wa habari,Msaidizi Kamishna wa Zimamoto, Iddi Khamis Juma, alisema vikosi hivyo vikiwa katika kazi zake za kawaida vilifanikiwa kukamata mafuta hayo majira ya saa 10:30 asubuhi ya kuamkia jana.
Alisema askari hao walikamata mafuta hayo baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema na kwa bahati mbaya hawakufanikiwa kuwakamata wahusika.
Alisema kikosi hicho kilichopo Mkumbuu, kimekuwa na kawaida ya kufanya doria kila pembe ya bahari, ambapo hivi karibuni walifanikiwa kukamata shehena ya mbao ambazo ziliingizwa kinyume na utaratibu na kuzifikisha mamlaka husika kwa hatua za kisheria.
Aliwapongeza wapiganaji hao kwa moyo wao wa kishujaa na wa kizalendo licha ya changamoto mbali mbali zinazowakabili.